MoCU yawavuta wananchi utoaji maoni uboreshaji huduma

23Jun 2022
Na Mwandishi Wetu
Moshi
Nipashe
MoCU yawavuta wananchi utoaji maoni uboreshaji huduma

CHUO Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), kimeibuka na mkakati mpya wa kuwafuata wadau wa elimu, hasa wananchi wa kawaida katika maeneo ya pembezoni na mijini ili kupata maoni yao kuhusu namna bora ya kuboresha huduma zake na kutatua matatizo yanayokikabili.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (TAALUMA), Prof John Safari (wa kwanza kushoto), alikabidhi sehemu ya vifaa vya kufanyia usafi wa mazingira kwa Mwenyekiti wa Soko la Manyema, Manispaa ya Moshi leo, kama sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma.

Akizungumza jana na wananchi, wafanyabiashara na wachuuzi katika Soko la Manyema, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), Prof. Alfred Sife, aliyekuwa ameongozana na watumishi wa chuo hicho kufanya usafi wa mazingira, alisema lengo lao ni kupata maoni ya wadau pamoja na watumishi wa umma.

“Kwenye maadhimisho ya mwaka huu ya wiki ya utumishi wa umma, iliyoanza Juni 16 na kuhitimishwa Juni 23, shughuli kubwa zilizofanyika ilikuwa ni kupata maoni ya watumishi wa umma, lakini na wadau wetu mbalimbali ambao tunafanya nao kazi ya kukusanya maoni kuhusu huduma zetu.

“Kwa sehemu kubwa tumeyakusanya kwa njia ya mtandao, tumetengeneza linki (utambulisho wa taarifa) kwenye social media (mitandao ya kijamii), ambayo tumeisambaza na watu wanaingia humo wanatoa maoni kuhusu huduma zetu, uzuri na matatizo yaliyopo katika huduma zetu.

“Wateja wetu wakubwa ni wanafunzi, lakini pamoja na kwamba tunafanya shughuli kufundisha, kufanya utafiti na kazi nyingine chuoni, tunafanya shughuli za kijamii pia. Tunafanya shughuli za outreach (huduma mkoba) na shughuli za jamii. Kwa hiyo kwa leo tukaona, tutoke tuje kwenye Soko la Manyema ili tushiriki kwa siku nzima kufanya usafi wa mazingira, kwa kushirikiana na uongozi wa soko, uongozi wa mtaa na ofisa mtendaji yupo na tumetoa taarifa Manispaa.”

Awali, Mkurugenzi wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu wa MoCU, Daudi Massambu, alisema kuwa la maadhimisho hayo ni kutambua mchango wa watumishi wa umma nchini.

“Kwa mujibu wa maelekezo ya serikali, maadhimisho haya hayakutakiwa kufanyika ofisini tu ila ni pamoja na kwenda kwenye maeneo ambayo ni ya pembezoni kupata maoni ya wananchi kwa sababu ndio wadau wakubwa na ndio waajiri wetu. Zoezi hili ni endelevu na mwaka ujao tutakuja tena,”alisema Massambu

Baada ya kufanya usafi sokoni, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (Taaluma), Prof. John Safari, aliwashukuru wananchi, wachuuzi, wafanyabiashara, viongozi wa soko hilo na serikali ya Mtaa, kwa kuungana nao kufanya usafi, huku akiwasihi kutochukulia mzaha suala la uzingatiaji wa kanuni za afya, hasa usafi wa mazingira kwa kuwa wao ni injini inayolisha maelefu ya watu Manispaa ya Moshi.

“Tunawashukuru sana viongozi wa soko  na serikali ya mtaa, mmetupa ushirikano huo na kimsingi soko hili ni letu sote kwa sababu tunapata hapa huduma za vyakula, lakini kwa leo tumekuja kwa namna tofauti kwa maana ya kufanya usafi wa mazingira. Tuendelee kuzingatia kanuni za usafi kama ambavyo zinatolewa mara kwa mara na seriakali. Vifaa tulivyokuja navyo tunawakabidhi na endeleeni kuvitumia,”alisema Prof. Safari

Naye, Mwenyekiti wa Mtaa wa Sokoni, Kata ya Bondeni, Mahamoud Ismail, aliwashukuru watumishi hao wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, akisema kwao wanaona kitendo hicho ni heshima, kwa sababu mazingira ya usafi wa soko hayakuwa rafiki.

“Kwa kweli tumefurahi sana watumishi wa umma kuja kufanya usafi na wananchi mtaani, kwetu tunaona ni heshima, kwa sababu mazingira ya usafi wa soko hayakuwa rafiki. Wametuonyesha mwangaza mzuri wafanyabiashara na wananchi wa Soko la Manyema. Tunaona wasiishie wiki ya utumishi wa umma, zoezi hili liwe endelevu,”alisisitiza Mwenyekiti huyo

Aidha, mfanyabiashara wa jumla na rejareja, Tumombe Emanuel, akieleza namna alivyoguswa na zoezi hilo alisema:

“Hadi watumishi wa umma kutoka darasani na kuja kutupiga jeki kufanya usafi ni fundisho kwetu wafanyabiashara. Tutaufuata utaratibu huu ili tufanye usafi kila siku na kuvutia wateja kutokana na usafi,

“Japo tatizo tulililonalo la usafi sokoni, tayari uongozi wa soko wamekuja na utaratibu wa kuchangia kuboresha usafi unaendelea, ingawa kuna maeneo michango inatofautiana, kwa sababu unakuta vigezo havizingatiwi vya kufanya usafi huo huo.”

Mwisho

Habari Kubwa