MOI yafanya upasuaji mkubwa wa ubongo

26Feb 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
MOI yafanya upasuaji mkubwa wa ubongo

MADAKTARI bingwa wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kwa kushirikiana na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking, nchini China, wamefanya upasuaji mkubwa wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo, kuziba mishipa ya damu iliyopasuka kwenye ubongo pamoja na ....

upasuaji wa mgongo.

Upasuaji wa uvimbe kwenye ubongo uliofanyika jijini Dar es Salaam, umechukua takribani saa tano.

Alisema, upasuaji huo umefuatia ujio wa jopo la madaktari bingwa watatu wa upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Peking cha China ambao waliwasili MOI wiki iliyopita, kwa lengo la kutoa mafunzo na kufanya kambi ya siku moja ya upasuaji.

Akizungumza katika chumba cha upasuaji MOI, Dk. Nicephorus Rutabansibwa, alisema ushirikiano kati ya MOI na Peking utakuwa wenye manufaa makubwa kwa sababu huduma zinazotolewa zitaendelea kuwa bora na Watanzania wataendelea kupata huduma hizo nchini bila ya kwenda nje ya nchi.

“Huu ni mwendelezo wa ushirikiano tulioingia na wenzetu hawa wa Peking mwaka jana, tunaamini tutabadilishana uzoefu na wenzetu hawa ambao wamepiga hatua kubwa kwenye teknolojia ya matibabu, kupitia ushirikiano huu, mbinu tunazopata zitatusaidia kuendelea kutoa tiba bora na kwa wakati kwa wagonjwa wetu,” alisema Dk. Rutabansibwa.

Dk. Rutabansibwa alisema jana waliwafanyia upasuaji wagonjwa watatu, akiwamo mmoja aliyefanyiwa wa kuondoa uvimbe kwenye ubongo kwa kutumia darubini ya kisasa, mwingine upasuaji wa mgongo na mwingine atafanyiwa upasuaji wa kuziba mishipa ya damu iliyopasuka kwenye kichwa.

Pia alisema ujio huo wa wataalamu kutoka Peking umelenga kuweka mazingira bora ya ushirikiano na MOI ili watakapo kuja tena wajue ni maeneo gani yanahitajika kuwa kipaumbele kwenye ushirikiano.

Kwa upande wake kiongozi wa jopo la madaktari bingwa kutoka Peking, daktari bingwa wa ubongo na mishipa ya fahamu, Profesa Yuanil Zhao, alisema ushirikiano kati ya MOI na Peking utakuwa wenye mafanikio makubwa na utawanufaisha wagonjwa pamoja na madaktari vijana ambao watapata fursa ya kusoma kwenye chuo chao.

“Tumefarijika kuja Tanzania, tumewaeleza hali halisi ya hospitali yetu na vifaa tulivyonavyo, tunaamini kupitia ushirikiano huu wataalamu wa hapa watajifunza na pia tutatoa fursa kwa wataalamu wawili hadi watatu kuja kujifunza kwetu,” alisema Profesa Zhao.

Kambi hiyo ni sehemu ya mwendelezo wa mkataba wa ushirikiano uliosainiwa kati ya MOI, Chuo Kikuu cha MUHAS na Hospitali ya Peking ya China ambao umejikita katika mafunzo ya muda mrefu na mfupi, utafiti, tiba pamoja na uboreshaji wa miundombinu.

Habari Kubwa