MOI yaokoa mtoto aliyetupwa

09Jul 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
MOI yaokoa mtoto aliyetupwa

TAASISI ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), imefanikiwa kuokoa maisha ya mtoto wa kike mwenye miezi miwili, ambaye alikuwa amejeruhiwa kichwani baada ya kutupwa na mama yake.

Mtoto huyo waliyempa jina la Precious Moi, alipokelewa MOI Juni 29, mwaka huu, akitokea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), baada ya kuokotwa na wasamaria wema.

Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi, aliiambia Nipashe jana kuwa, mtoto huyo aliokotwa maeneo ya Tegeta akiwa ametupwa.
“Alifikishwa MOI akitokea Muhimbili baada ya kupata majeraha maeneo ya kichwani na tulipompokea alikuwa na hali mbaya, alikuwa ameumia zaidi maeneo ya kichwani kiasi kwamba alikuwa hawezi kufumbua macho,” alisema Mvungi.

Alisema walianza kufanya uchunguzi wa kina na kumpatia matibabu kuanzia siku hiyo hadi hali yake ilipotengamaa.

“Kwa sasa anaendelea vizuri, baada ya kumpatia tiba na lishe ya kutosha kwa kushirikiana na watoa huduma wetu wa MOI,” alisema Mvungi.

Kadhalika, Mvungi alisema watumishi wa hospitali hiyo, waliguswa na historia ya mtoto huyo, wakachanga fedha kwa ajili ya kumnunulia mavazi na kumpatia huduma nyingine muhimu za mtoto.

MOI pamoja na kumtibia kwa mfumo wa kundi la msamaha wa matibabu pia wanagharamia maziwa yake kwa kipindi chote akiwa hospitalini hapo.

“Mtoto huyu aliwagusa watumishi wa MOI walimnunulia nguo za kutosha, nepi na MOI tunamhudumia maziwa na matibabu baada ya hapo tutamkabidhi kwenye kituo cha kulea watoto yatima,” alisema.

Kutokana na mtoto huyo kutokuwa na ndugu wa kumlea, Mvungi alisema waliamua kumpatia jina la Precious MOI na baada ya hali yake kuimarika vyema watampeleka kwenye kituo cha kulelea watoto yatima.

Wasamaria wema waliomwokoa mtoto huyo hawajafuatilia hali yake, ndiyo sababu MOI imeamua kumpeleka kituo cha kulelea yatima.

Habari Kubwa