Mongela ataka nguvu itumike dhidi ya wabakaji

29Nov 2020
Richard Makore
Mwanza
Nipashe Jumapili
Mongela ataka nguvu itumike dhidi ya wabakaji

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela, ameliagiza Jeshi la Polisi mkoani humo kutumia nguvu katika kupambana na watu wanaofanya vitendo vya ukatili wa kijinsia, ikiwamo kuwabaka watoto na kuwapa mimba.

Mongela alisema hayo jana wakati wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa jinsia, yaliyofanyika jijini hapa na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.

Alisema mikoa ya Kanda ya Ziwa ina takwimu za juu kuhusu vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake, kwamba nguvu za ziada zinahitajika kupambana navyo.

Mkuu huyo wa mkoa aliitaka jamii kufichua vitendo vya ukatili wa kijinsia badala ya kuvifumbia macho, kwa kuwa vinaathiri maisha ya watu wanaofanyiwa hivyo.

Kutokana na hali hiyo, alimwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Muliro Jumanne, kusimamia suala hilo, ili kulikomesha na kwamba ikiwezekana wawapoteze wabakaji.

Alisema juhudi za kupambana na vitendo hivyo zinarudishwa nyuma kutokana na badhi ya wazazi ambao wanakubali kupokea zawadi kutoka kwa wahalifu ili wamalize kesi nje ya mahakama.

Kamanda Muliro aliahidi kutumia nguvu kupambana na watu hao kama wanavyofanya katika mapambano dhidi ya majambazi.

“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa agizo lako tutalitekeleza kwa nguvu nyingi bila uoga ili kukomesha ukatili wa kijisnia kwenye jamii,'' alisema Kamanda Muliro.

Naye Mkuu wa Dawati la Jinsia la Polisi mkoani Mwanza, Faraja Mkinga, alisema mwaka huu matukio 1,387 yameripotiwa.

Aliongeza kuwa kesi 455 zilifikishwa mahakamani ingawa baadhi ya watu waliofanyiwa ukatili wa kijinsia wanashindwa kutoa ushirikiano kwa kutoa ushahidi.

Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini ambalo linatoa msaada kwa watoto wanaofanyiwa ukatili, Yassin Ally, alisema vitendo hivyo bado vinaisumbua jamii.

Habari Kubwa