Moto unavyoitesa hifadhi Mlima Kilimanjaro

07Jun 2021
Jenifer Gilla
KILIMANJARO
Nipashe
Moto unavyoitesa hifadhi Mlima Kilimanjaro

​​​​​​​KILOMETA 45 kutoka Moshi mjini, sawa na mwendo wa takribani nusu saa kwa usafiri wa gari, ndipo unapatikana Mlima Kilimanjaro.

WAFANYAKAZI WA KINAPA WAKIZIMA MOTO KWENYE ENEO LA MLIMA KILIMANJARO.

Ni mlima unaojizolea sifa ya ukubwa kuliko yote barani Afrika na wa pili duniani, ukinakshiwa na miti ya asili ya aina yake pamoja na viumbe hai kama vile mbega, nyani, nyati, chui, tembo, swala na ndege, ambao huongeza vionjo kwa watalii kutoka mataifa mbalimbali wanaokuja kuupanda na kujiwekea rekodi.

Licha ya sifa kubwa iliyonayo mlima huo ulimwenguni, kwa miaka mingi umekuwa ukiandamwa na jinamizi la kuungua moto ambalo linachangia kushusha hadhi yake siku hadi siku.

Nipashe ilifunga safari hadi Makao Mkuu ya Hifadhi ya Mlima huo (KINAPA), iliyopo Marangu, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro na kufanya mahojiano na mamlaka hiyo kufahamu kinachojiri juu ya suala hilo.

Imani Kikoti,ni Ofisa Uhifadhi Mkuu anayesimamia Idara ya Sayansi na Uhifadhi katika mamlaka ya hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), anayetoa simulizia kuwa kwa muda mrefu hifadhi hiyo umekua ukiandamwa na majanga ya moto ambayo kwa kiasi kikubwa husababishwa na shughuli za kibinadamu.

Chanzo cha moto

Kikoti anathibitisha kwa kujiamini kuwa katika uchunguzi walioufanya walibaini kuwa hakuna moto wa asili uliotokea katika hifadhi hio, yote husababishwa na shughuli za binadamu.

“Moja ya shughuli zinazosababisha kuzuka kwa moto kwenye hifadhi ni uvutaji wa sigara unaofanywa na watalii pamoja na wasaidizi wao, ambao baada ya kumaliza hutelekeza vipisi vya sigara vikiwa na moto ambavyo husambaa kupitia majani makavu.

Pia wasaidizi wanapowasha moto na kupikia watalii chakula hawazimi moto ule vizuri wanapomaliza shughuli hiyo hivyo husambaa na kuleta majanga” anasimulia Kikoti.

Sababu nyingine anataja ni uwindaji haramu ambapo mwindaji anapokamata mnyama anaamua kumchoma msituni kwa kuhofia kukamatwa kwa kosa la kuwinda bila kibali cha mamlaka.

Anataja pia urinaji wa asali kuwa ni chanzo cha kuzuka moto msituni kwa kuwa wanakjiji wanarina kizamani kwa kutumia moto kufukuza nyuki ambao husambaa na kuunguza msitu.

Njia ya uandaaji mashamba ya kizamani kwa kutumia moto anaitaja kuwa ni chanzo cha moto katika hifadhi kwa masahamba yaliyo karibu na hifadhi hiyo ambapo moto unaochomwa katika mashamba hayo kwa ajili ya kuunguza visiki husambazwa na upepo hadi kwenye hifadhi.

Athari

Kwa mujibu wa Kikoti, moto unasababisha kupungua kwa miti katika hifadhi hiyo ambayo ndio tegemeo kuu la kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi yanayoiathiri dunia.

Mhifadhi huyo anakiri kuwa mpaka theruji ya mlima Kilimanjaro imepungua hadi kufikia kilometa za mraba 1.76 chanzo kikuu kikiwa ni ongezeko la joto linalotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

“Tunategemea miti hii ili kuunusuru mlima kuendelea kuyeyuka na kupoteza mvuto wake, hivyo moto unaowaka kila mara unarudisha nyuma juhudi zetu” anasema Kikoti .

Athari nyingine kwa mujibu wa Kikoti inaangukia kwa viumbe hai wanaotegemea msitu huo kwa makazi ambao hulazimika kukimbia kuhama makazi pale moto unapowaka.

“Mnyama kama ndezi au swala ambao hula majani wanaathirika sana mto unapowaka kwa kuwa wanakosa chakula, kwa hiyo kuhama makazi kutafuta chakula , wengine hutoka nje ya hifadhi kabisa kwa kupitia mashoroba na kwenda kwenye bhifadhi nyingine kama vile Serengeti” anasimulia kikoti .

Mwenyekiti anena

Mwenyekiti wa Kijiji cha Msiri, Kata ya Marangu Mashariki, John Mtui anayekiri kuwa moto unapowaka mlimani kunakuwa na hofu kubwa kwa wananchi hali inayopelekea wengine kuondoka kwa muda.

“Unajua kijiji hichi kipo mpakani kabisa na mlima, hivyo moto unapowaka kwa upande wetu huwa tunausikia kabisa hivyo kunakuwa na taharuki na hofu inatawala kuwa huenda unaweza kufika kwenye nyumba zetu usiku na kutuunguza”, anasimulia

Hata hivyo kiongozi huyo wa kijiji kwa kushirikiana na idara ya ulinzi na uokoaji ya KINAPA, wanafanya kazi kubwa ya kuwatoa hofu wanakijiji pamoja na kuhakikisha wanachukua kila tahadhari ili moto usifike kwenye makazi ya watu.

“Tunahakikisha hawaendi msituni kipindi chote moto unapowaka ili kuwaepusha na majanga yanayoweza kusababishwa na mto huo” anasema Mtui.

Wanakijiji walia

Katazo la kuingia msituni pindi moto unapokuwa unawaka hugeuka shubiri kwa wananchi hao ambao hutegemea msitu huo kwa shughuli mbalimbali.

Mesia robson (31), mkazi wa kijiji cha Msiri analalamika kuwa moto husababisha mifugo yake kukosa chakula na hata kufa kwa kuwa hutegemea kukata majani kwenye msitu huo.

“Kuna mbuzi wangu mwaka jana alizaa watoto wakafa kutokana na kukosa lishe, kwa sababu tulikaa wiki mbili bila ya chakula cha kutosha kwa kuwa moto ulikuwa unawaka msituni” anasema.

Wakati mary shayo akalalamikia moto huo kusababisha uhaba wa kuni kwa kuwa hutegemea kuni katika hifadhi hiyo na kusababisha kununua kwa watu ambao huuza bei ya juu.

“Unalazimika kununua wa walio nazo ambapo mtu anakuuzia fungu moja sh.2000, kwa kuwa unashida utanunua tu, kwa sisi wenye mahindi ndani tunatumia magunzi.

Athari kiuchumi

Wanakijiji hao pia hulalamikia shughuli za kiuchumi kusimama kutokana na watalii kusitisha kupanda mlima kama anavyosimulia mpagazi Munguatosha Mosha (32)

“Kwa sisi wasindikiza watalii inakuwa ni hatari kwa sababu zile shughuli zinakufa na ndio ajira zetu, na sio kwamba moto ukidhibitiwa tu ndio watalii wanaruhusiwa hapana, hapo mtakaa hata mwezi ili kujiridhisha”.

Kwa safari moja inayohusisha siku saba john hulipwa ujira sh. 100,000 hadi 150, kutegemea na kampuni iliyompa kazi.

Alphonce shayo (35), muuza duka la vitu vya asili katika geti la kupandia watalii la Marangu anasimulia kupata hasara ya takribani Sh. 50,000 kwa siku, pindi moto unapowaka kwenye hifadhi hiyo kutokana na kutokuwapo na watalii wa kuwauzia.

“Huwa ninawauzia vitu vya asili ya Tanzania kama vile shanga, vinyago, picha za mlima, na tunawapatia hapa wanapokuwa wanaelekea kupanda mlimani, sasa kunapotokea majanga ya moto hawaji tena” anasema.

Kilio hadi serikalini

Moto huo pia umekuwa ukiitia serikali harasa kwa kuharibu miundombinu pamoja na majengo yalipo ndani ya hifadhi.

Akitoa tathmini ya athari za moto uliotokea Oktoba, mwaka jana katika hifadhi hiyo, aliyekuwa Waziri wa utalii na Maliasili, Dk.Hamisi Kigwangala alisema uliteketeza mabanda ya kupumzikia wageni 12, kumi yakiwa ya wageni wa kawaida na mawili ya wageni maalum ambayo ndio yalikuwa yamekamilika kujengwa kisasa.

Aliongeza kuwa moto huo uliunguza mitambo ya umeme wa jua pamoja na vyoo viwili.Hali itakayoigharimu serikali kuingiza mkono mfukoni na kufanya matengenezo kwenye uharibifu huo.

Naye Mhifadhi Mkuu Kikoti anakiri kuwa majanga ya moto yanaitia hasara serikali kwa kuwa shughuli za utalii zinaposimama kutokana na majanga hayo serikali inakosa pato linalotokana na kodi hiyo.

Kwa mujibu wa mhifadhi huyo, wanapokea wastani wa watalii 5000 kwa mwaka ambao serikali hupokea kodi kutoka kwa kila mtalii.

Uwapo wa watalii hao pia  husababisha kupatikana kwa ajira kwa vijana wa eneo hilo, ambapo mhifadhi Kikoti anathibitisha kuwa kila mwaka vijana 2500 wanapata ajira ya kwa kuwa kila mtalii mmoja anatakiwa asindikizwe na mpishi mmoja, wapagazi watatu na mwongoza watalii mmoja.

Mabadiliko ya tabia nchi

 Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam katka Taasis ya Tathmini ya Rasilimali, Dk. Noah Makula anatoa ushuhuda jinsi uchomaji wa moto unavyochangia mabadiliko ya tabia nchi akisema:

“Miti inanyonya na kuhifadhi  hewa chafu inayoitwa ‘carbon dioxide sink’, inapochomwa  hiyo hewa inatoka na kuelekea angani na kuathiri tabaka la ozone, ambapo kuharibika kwa tabaka hili kunasababisha kupenya kwa miale ya joto kutoka angani na kusababisha joto kuongezeka.

Kwa mujibu wa ripoti ya jopo la wanasayansi wa Utafiti wa Athari za Mabadiliko ya Tabianchi  (IPCC) juu ya athari ya ongezeko la joto, kwa sasa joto limeongezeka na kufikia nyuzi joto 15, na juhudi za haraka zinahitajika ili kuizuia isifikie nyuzijoto 2.

Wakati huo huo  taarifa za kisayansi  zinasema kuwa gesi ya aina ya carbon dioxide( Co2) ndio inaongoza kwa kuathiri tabaka la ozone  kwa asilimia 66, ikifuatiwa na methale(CH4) asilimia 15.

Changamoto katika uzimaji

Ofisa Uhifadhi Mwandamizi anayesimamia Idara ya Ulinzi na Uokoaji, Mapinduzi Ndesa anayesimulia kuwa idara yake inapitia changamoto mbalimbali katika kukabiliana na moto unapozuka kwenye hifadhi.

Anataja mojawapo uhaba wa vifaa vya kisasa vya kukabiliana na moto huo ambavyo hufanya shughuli hiyo kuchukua muda mrefu tofauti na matarajio yao.

“Hatuna vifaa vya kisasa vya kuzimia moto vinavyoweza kudhibiti kasi ya moto inayochochewa na upepo, sisi tunatumia magari ya zimamoto, na njia za kawaida za kutumia ndoo za maji na michanga hali ambayo haisaidii kitu.

“Pia hata magari yenyewe yanashindwa kufika eneo la tukio mapema kutokana na changamoto ya njia, kwa sababu kwenye huu mlima kuna sehemu ikifika magari hayawezi kupita inabidi tulazimishe njia yanapotokea majanga” anasimulia.

Changamoto nyingine kwa mujibu wa Ndesa ni kutokuwa na wataalamu wa kutosha wa uzimaji wa moto ambao wanasababisha nguvu kazi kuwa ndogo pale majanga yanapotokea.

“Tukizidiwa sana inabidi tuombe nguvu kazi kutoka kwa wanakijiji ambao hawana elimu kuhusu kuzima moto kwa hivyo inabidi askari wawe nyuma yao kuhakikisha wanakuwa hawapati madhara”, anamalizia kwa huzuni.

Mara ya mwisho mlima huo kuwaka moto ilikuwa ni Oktoba, mwaka jana na kusababisha hekta 22.5 kuteketea, akisema juhudi za kuzima moto huo zilichukua takribani wiki mbili.

WADAU WAONGEZA NGUVU

Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kaskazini ,Lewis Nzali, ambao ndio wasimamizi wakuu wa mazingira kikanda anasema huwa wanaongeza nguvu kwa KINAPA wakati wa kupambana na janga hilo.

“ Huwa hatuwaachi, tunatuma nguvu kazi ikiwamo vifaa vi kiwamo magari ya kuzimia moto, tunatoa vifaa vya kujikinga pamoja na wataalamu wa majanga ya moto ili kuongeza nguvu, na kama tukiona tumezidiwa tunakaa pamoja kama timu na kujadili nini kifanyike” anasema.

Usikose sehemu yapili ya makala hii unayoongelea jinsi KINAPA na wadau wengine wanavyopambana kumaliza tatizo la upunguaji wa miti katika hifadhi hiyo.

Habari Kubwa