Moto wateketeza hoteli nne, watalii waokolewa

21Nov 2021
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe Jumapili
Moto wateketeza hoteli nne, watalii waokolewa

​​​​​​​BAADHI ya watalii wamenusurika kifo baada ya hoteli walizofikia huko Jambiani, Mkoa wa Kusini Unguja kuteketea kwa moto uliozuka juzi majira saa 11:00 jioni.

Moto ukiteketeza hoteli nne za kitalii katika eneo la Jambiani, Mkoa wa Kusini Unguja juzi jioni. PICHA: MPIGAPICHA WETU

Moto huo umeteketeza hoteli nne ambapo tatu kati ya hizo, hakuna kilichotolewa zaidi ya watalii waliokuwamo.

Akizungumza na Nipashe jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, Suleiman Hassan, alisema moto huo ulianza kuteketeza hoteli ya Villa de Coco kisha kuzifikia hoteli zingine zilizoko karibu.

Alizitaja hoteli hizo ni Spice Island ambayo imeungua vyumba sita vya kulala wageni, Fun Beach na Cobe ambazo zimeteketea zote.

Kamanda Hassan alisema chanzo cha moto huyo bado hakijajulikana, lakini taarifa za awali zinadaiwa kuwa ni hitilafu ya jiko katika hoteli ya Villa de Coco.

Alisema katika ajali hiyo ya moto hakuna kifo wala majeruhi kwa sababu watalii

waliokuwapo katika hoteli hizo, waliokolewa haraka na kuhifadhiwa katika hoteli ya Shaharzade.

“Tunashukuru kuwa hakuna kifo wala majeruhi wa moto huu, watalii wote pamoja na wafanykazi wa hoteli hizi waliwahi kutoka. Bado thamani ya gharama ya vitu vilivyoteketea katika hoteli hizi haijajulikana," alisema.

Alifafanua kuwa moto huo ulikuwa mkubwa kutokana na paa la hoteli kuezekwa kwa makuti, lakini ulidhibitiwa majira ya saa mbili usiku juzi.

Kamanda Hassan alisema kila hoteli ina mmiliki tofauti, wote wakiwa ni rai wa kigeni na hana uhakika kama hoteli hizo zimekatiwa bima.

Baadhi ya mashuhuda waliokuwapo katika ajali hiyo, walisema kuwa moto huo haukudhibitiwa mapema na ndio sababu ukasambaa na kuteketeza hoteli zingine.

Habari Kubwa