Moto wateketeza makazi ya mapadri

18Jan 2019
Na Waandishi Wetu
Nipashe
Moto wateketeza makazi ya mapadri

MOTO ambao chanzo chake bado hakijafahamika, umeteketeza makazi ya mapadri wa Kanisa Katoliki maeneo ya Segerea, jijini Dar es Salaam.

Mapadri hao ambao wanaishi kwenye nyumba za walimu wa Seminari ya Mtakatifu Karol Lwanga ya Segerea, hata hivyo, hawajapata madhara yoyote licha ya makazi hayo kuteketea.

Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk. Charles Kitima, alisema kuwa chanzo cha moto huo hakijajulikana na wanashukuru mapadri wote wamesalimika isipokuwa vitu vyao ndivyo vimeteketea.

“Ni nyumba ya makazi ya mapadri walimu…vyumba 12 vya juu vyote vimeteketea, tunasubiri taarifa kutoka kwa wahusika kujua chanzo cha moto huo na tunashukuru kikosi cha zimamoto kilisaidia kuudhibiti hivyo haukufika kwenye vyumba vya chini,” alisema Dk. Kitima.

Alisema siku mbili kabla ya tukio hilo, kulikuwa na hitilafu ya umeme katika eneo hilo na wahusika walitoa taarifa Shirika la Umeme (Tanesco), ambao walifika na kufanya uchunguzi.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Elisa Mugisha, alisema kuwa walipata taarifa za kuzuka kwa moto huo juzi saa 5 usiku na haraka walikwenda kwenye eneo la tukio ili kuzima moto huo.

Alisema walipofika huko walikuta moto mkali hivyo waliwasiliana na viongozi wa kikosi hicho Mkoa wa Temeke ili kuongeza nguvu.

Kitima alisema bado moto ulizidi kupamba hivyo waliamua kuwasiliana na kikosi kilichopo uwanja wa ndege ndipo wakafanikiwa kuuzima saa 6.50, usiku huo.

“Taarifa za awali tulizopata ni kwamba moto huo ulianzia kwenye chumba cha Padri Benedict Shemfumbwa, ambaye hakuwa ndani, tunaendelea kukusanya taarifa za uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto, ingawa inasadikiwa ni hitilafu ya umeme,” alisema Kamanda Mugisha.

Msemaji wa Tanesco, Leila Muhaji, alisema baada ya kuitwa walibaini kwamba kuna tatizo kwenye mfumo wa ndani wa umeme katika jengo hilo hivyo wakawashauri washughulikie.

“Mhandisi wetu wa Ilala amenihakikishia kuwa tatizo halikuhusiana na miundombinu yetu, tunashiriki kuhakikisha kwamba madhara hayatokei zaidi kwa kusaidia kutofautisha mfumo huo ili kuepusha madhara mengine zaidi,” alisema Leila.