Mpango akerwa taka jiji la Dodoma

16Jan 2022
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe Jumapili
Mpango akerwa taka jiji la Dodoma

MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango, ameeleza kukerwa na taka katika jiji la Dodoma na kutoa wiki mbili kwa uongozi wa jiji hilo kuondoa taka zote zilizozagaa mitaani.

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango akiangalia lundo la takataka zilizotelekezwa nje ya soko kuu la Majengo, jijini Dodoma jana, alipofanya ziara ya kushtukiza kukagua hali ya usafi katika eneo hilo, ambapo alitoa muda wa wiki mbili ziwe zimetolewa. PICHA: OMR

Sambamba na hilo, amemwagiza Mkurugenzi wa Jiji hilo kuvunja mkataba na Kampuni ya Usafi wa Mazingira ya Green Waste.

Alitoa maagizo hayo baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kukagua usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya Soko la Majengo na kubaini kuwapo kwa mlundikano wa taka nyingi.

Dk. Mpango alisema ni aibu kwa Jiji la Dodoma ambalo ndilo makao makuu ya nchi kuwa na mlundikano wa uchafu katika maeneo ya masoko ambayo yanatumiwa na watu kufanya biashara mbalimbali za vyakula.

Pia aliwaagiza wakurugenzi wa majiji yote nchini kuhakikisha suala la usafi linapewa kipaumbele na kuwa endelevu.

“Jiji la Dodoma ni chafu sana mnashindwa hata na Dar es Salaam. Wao wako vizuri na kule ndiko kuna fujo sana. Kwa mfano barabara hii ya kutoka Arusha pembezoni kumejaa taka. Sasa ndani ya wiki mbili nataka msafishe kote na mimi bahati nzuri nakaa hapa Dodoma lazima nitakuja kukagua,”alisisitiza Dk. Mpango.

Kuhusu kampuni ya usafi ya Green Waste alimtaka Mkurugenzi wa Jiji kuvunja mkataba na kampuni hiyo baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru, alisema moja ya changamoto wanayokabiliana nayo ni uhaba wa magari kwa ajili ya kuzoa taka hizo.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka, alisema atahakikisha kuwa maagizo ya Makamu wa Rais yanafanyiwa kazi.

“Tutahakikisha kuwa tunatekeleza maagizo yote katika muda uliotupatia na leo hii viongozi wote wa jiji na wilaya watabaki hapa kufanya vikao ili kupata suluhu ya kuziondoa taka hizi,” alisema Mtaka.

Habari Kubwa