Mpango alitaka Shirika la Posta lijitathmini upya

10Oct 2021
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe Jumapili
Mpango alitaka Shirika la Posta lijitathmini upya

MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango, amelitaka Shirika la Posta Tanzania kujitathimi na kuzifanyia kazi dosari mbalimbali zilizopo ili kuukabili ushindani wa soko katika sekta ya usafirishaji wa mizigo na vipeto ulipo hivi sasa duniani.

Dk. Mpango aliagiza hayo jana jijini Dodoma alipofunga maadhimisho ya Siku ya Posta Duniani.

"Hatuna budi kujitathmini kwa huduma zetu za Posta kama zinazingatia vigezo. Vilevile, tujipime vizuri kama huduma zetu zinaendana na maendeleo yaliyofikiwa na nchi yetu katika uchumi wa kati," alisema Dk. Mpango.

Alisema moja kati ya dosari ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi ni pamoja na matumizi ya fursa za kibiashara zilizopo nje ya nchi hasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na ile ya Maendeleo Kusimi mwa Afrika (SADC), ambazo bado hazijatumiwa vizuri na shirika hilo.

"Takwimu za huduma za Posta zinaonyesha kuwa huduma za Posta zinachangia chini ya asilimia 0.5 ya fedha za kigeni zitokanazo na mauzo ya huduma za Posta nje ya nchi huku tukiwa na fursa kubwa ya biashara katika jumuiya zetu,”alisema.

Dk. Mpango alilitaka shirika hilo kuongeza jitihada za kutangaza huduma zake ili jamii ipate kuelewa taswira mpya ya shirika nchini.

“Jana nilitembelea tovuti yenu, nikakuta iko katika lugha ya Kiingereza. Nani atawaelewa? Ninawaagiza sasa muweke pia katika lugha ya Kiswahili ili Watanzania wengi wapate kutambua huduma mnazozitoa," aliagiza.

Dk. Mpango pia alisema hivi sasa huduma za Posta zinakabiliwa na ushindani mkubwa, hivyo ili ziendele kuwa endelevu, ipo haja ya kuwapo kwa ubunifu.

“Ili huduma hizi ziendelee kuwa endelevu kuna haja ya kuwa wabunifu na kukidhi mahitaji ya wateja, ni lazima twende sawa na mabadiliko ya TEHAMA na mahitaji ya sasa ya dunia yanataka nini," alisema.

Kiongozi huyo wa serikali alibainisha kuwa kwa mujibu wa utafiti wa Benki ya Dunia (WB) wa mwaka 2004, ukuaji wa huduma za Posta unachochea ukuaji wa pato la mtu mmoja mmoja.

“Huduma za Posta zinatakiwa kuwa za uhakika ili kujenga imani kwa wateja, ikiwa ni pamoja na kuzingatia muda, usalama wa vitu vinavyotumwa. Pili, huduma zitolewe kwa ufanisi, kwa gharama nafuu na ubora wa hali ya juu”alisisitiza.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Ashatu Kijaji, alisema mashirika ya Posta duniani yamewekeza katika teknolojia wakati huu ambapo dunia inakabiliwa na janga la UVIKO-19.

Katika maadhimisho hayo, Dk. Mpango alikabidhi vitendea kazi vya magari na pikipiki kwa Shirika la Posta Tanzania ili kuliwezesha kuongeza ufanizi katika utekelezaji wa majukumu yake mbalimbali.

Habari Kubwa