Mpango, Majaliwa, Ndugai wawafunda mawaziri wapya

14Sep 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mpango, Majaliwa, Ndugai wawafunda mawaziri wapya

VIONGOZI wakuu serikalini wameeleza namna mawaziri walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan juzi, walivyo na kibarua cha kuwatumikia Watanzania kwenye sekta mbalimbali.

Mawaziri wanne na Mwanasheria Mkuu wa Serikali walioteuliwa wakila kiapo cha uadilifu kwa viongozi wa umma katika hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma jana. PICHA: IKULU

Mawaziri  ni Dk. Stergomena Tax wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT); January Makamba  wa Nishati; Dk. Ashatu Kijaji wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Prof. Makame Mbarawa wa Ujenzi na Uchukuzi.

Mbali na mawaziri mteule mwingine wa Rais Samia ambaye pia aliapishwa jana ni na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Eliezer Feleshi.

Akizungumza kwenye uapisho wa viongozi hao, Spika wa Bunge Job Ndugai, alisema Bunge ni kama chuo watu wamekuwa wakipanda na wengine kushuka na wengine wakipotea.

Alisema Prof. Mbarawa wizara aliyopewa ni kubwa na imebeba sehemu kubwa ya bajeti ya serikali na kuahidi Bunge litamsaidia.

“Dk. Tax umepewa kibubu nyeti kabisa cha ulinzi Mungu akutangulie, ni imani kubwa sana ya Rais kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri wa Ulinzi umeaminika sana, Dk. Ashatu kwenye teknolojia ya habari dunia ya sasa ipo hapo kwako utusaidie sana, mabadiliko ya teknolojia ni muhimu sana kwenye nchi yetu na hasa kwenye kupunguza gharama za uendeshaji wa serikali,” alisema.

Alisema Mabaraza ya Madiwani nchini yanatumia makablasha ya makaratasi na kama ikianzishwa mifumo ya TEHAMA itasaidia kupunguza gharama kwa kiwango kikubwa na kupunguza idadi ya vikao.

Kuhusu Nishati, Ndugai alisema ni eneo la kipekee na nyeti na kwamba wakati Makamba akiwa Mwenyekiti wa Kamati alifanya kazi nzuri.

“Kipindi kile tulibaini serikali ina madeni makubwa na mikataba mibovu ya eneo la nishati, serikali imejitahidi sana endelea kututoa huko ili tuwe na mikataba bora ya nishati hasa ya umeme, tuna tatizo kwenye nishati ya petroli na jamii zote ni matarajio mtaenda kuliangalia hilo pia na bei ya petroli isipande kama inavyokwenda tuangalie mbinu mbadala kwenye eneo hilo,” alisema.

 “Eneo la gesi hapa katikati hatukulipa heshima yake ni eneo la utajiri lazima eneo la gesi lifanyiwe kazi na nchi ipate mapato ya kutosha, pia Liganga Mchuchuma ni moyo wa nchi limezungumzwa sana huko nyuma hebu tukazalishe umeme pale, tukifanikiwa tutafika mbali, ukifanya kazi vizuri (Makamba) unatutoa hapa tulipo,” alisema.

Naye, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, alimtaka Waziri Makamba kusimamia miradi mikubwa kwenye sekta yake isikwame hata kidogo.

“Mradi wa umeme vijijini,tupa jicho kwa watendaji wa TANESCO, angalia maeneo ambayo gridi ya umeme haijafika,Mbarawa kawasimamie makandarasi na TANROADS ,huko kwenye usafiri wa majini miradi tuliyoahidi, itekelezwe na kukamilika,” alisema.

Hata hivyo, alisema Mwanasheria Mkuu anaifahamu serikali kuna kero nyingi sana anaamini atasaidia kukwepa matatizo mengi waliyokuwa nayo kwenye mikataba mbalimbali.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema wao kama wasaidizi wa Rais wanalo jukumu la kujifunza mwelekeo na matakwa ya Rais kwenye eneo waliomo ili kila mmoja awajibike kikamilifu.

“Mawaziri wenzangu karibuni tumewapokea kwa mikono miwili, naamini tutakaa pamoja kufanya mapitio ya maeneo mengine, lakini katika kipindi hiki niwasihi pale ambapo mtakabidhiwa majukumu na wale waliowatangulia mtaendelea kuzisoma na kuzielewa vizuri wizara zenu ili tuweze kufanya kazi kwa weledi, niendelee kukuahidi tutaendelea kuwajibika ipasavyo kwa weledi na kwa uaminifu mkubwa ili kuhakikisha serikali yako inatoa huduma, inatekeleza malengo yako na kuwafikia Watanzania popote walipo,” alisema  Waziri Mkuu.

Aidha alimkumbusha Mwanasheria Mkuu wa Serikali jukumu lililopo la kufanya kazi kwa pamoja na bunge ambapo alisema “Bunge linatupa majukumu mengi, linatushauri mambo mengi, lakini pia mengi ni ya kisheria na wewe ndiye hasa upo kwenye dawati hilo ikiwamo na maazimio yote ya Bunge, mikataba inahitaji kupitiwa kwa haraka kwa uhakika ili ifanyiwe maamuzi tuweze kutekeleza ushauri na maagizo wakati mwingine ya Bunge ili serikali iweze kufanya kazi yake vizuri.”