Mpango wa diaspora kupewa hadhi maalum wafikia pazuri

13Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mpango wa diaspora kupewa hadhi maalum wafikia pazuri

SERIKALI imesema iko katika hatua ya uchambuzi wa maoni kwa ajili ya kukamilisha mchakato wa hadhi maalum kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora).

Baada ya kukamilika kwa uchambuzi huo, maoni hayo yatawasilishwa bungeni kwa lengo la kuwawezesha Watanzania hao kushiriki na kuchangia kikamilifu maendeleo ya nchi yao ya asili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, alisema hayo kauli hivi karibuni wakati akizungumza na Jumuiya ya Watanzania waishio nchini Italia.

Alisema tayari mchakato wa awali wa kukusanya maoni kutoka kwa wadau wote, wakiwamo diaspora umekamilika na sasa wataalamu wako katika hatua za uchambuzi wa maoni hayo.

Kwa mujibu wa Balozi Mulamula, mchakato wa hadhi maalum utakapokamilika, utatoa haki za kiraia kwa Watanzania waishio nje ya nchi isipokuwa kushiriki katika siasa kwa kuwa suala hilo linahitaji mapitio ya kikatiba.

Pia alisema Rais Samia Suluhu Hassan anatambua mchango wa diaspora katika kujitafutia maendeleo yao na kuwataka kuendelea kuwa wazalendo kwa kushiriki kuijenga nchi kwa kuitangaza vyema kibiashara na kuleta wawekezaji kwenye sekta mbalimbali na kuleta ujuzi.

Akizungumza kwa niaba ya Watanzania waishio nchini Italia, Anastazia Lubangula, alisema wanaunga mkono hatua ya serikali ya kuanzisha mchakato wa kuwapatia hadhi maalum kwa kuwa itawawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi kwa kuaminiana.

Pia waliiomba serikali kuangalia upya suala la kuwawezesha kufungua akaunti katika benki za Tanzania kwa kuwa sheria inayosimamia suala hilo inawanyima haki ya kujiwekea akiba nyumbani kupitia benki na kwamba inainyima nchi mapato.

Sambamba na hilo, wamempongeza Rais Samia anavyoendesha shughuli za kiutawala tangu aingie madarakani miezi sita iliyopita na kwamba wana imani uongozi wake kuwa utaondoa mikwamo na kuimarisha uhusiano na mataifa na taasisi za kimataifa kwa maendeleo ya Tanzania.

Waziri Mulamula katika ziara yake nchini Italia, alishiriki mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na Italia, mkutano wa kimataifa wa amani pamoja na kukutana kwa mazungumzo na viongozi wa taasisi za kimataifa likiwamo Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD).