Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wahitaji trilioni 107/-

21Apr 2016
Na Waandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wahitaji trilioni 107/-

SHILINGI trilioni 107 zinahitajika kugharimia utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano, 2015/16 hadi 2020/21.

Aidha, Serikali ya Awamu ya Tano imesisitiza itaendelea na mwendo wake wa 'kutumbua majipu' ikiamini ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kunakuwa na nidhamu katika rasilimali za taifa.

Akiwasilisha mpango huo bungeni mjini hapa jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema serikali iatatumia Sh. trilioni 21.4 kila mwaka kukamilisha kutekeleza mpango huo.

Dk. Mpango alisema katika mpango huo, serikali itachangia Sh. trilioni 59 (sawa na Sh. trilioni 11.8 kila mwaka), huku akisema wamejiridhisha kutakuwa na ongezeko kubwa la fedha zinazohitajika kugharamia mpango huo ikilinganishwa na ule wa kwanza.

Alisema mpango huo umelenga kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu na kufikia malengo ya serikali ya kupunguza umaskini.

Alieleza kuwa serikali itaendelea na utaratibu wake wa 'kutumbua majipu' wakiamini ndiyo dawa ya kukuza uchumi wa nchi kwa vile kutakuwa na nidhamu ya matumizi.

Alisema Tanzania ambayo ina miaka zaidi ya 50 tangu ipate uhuru wake, sasa haihitaji tena kuendelea kuwa ombaomba.

Hata hivyo, Dk. Mpango alikiri maisha bado ni magumu kwa wananchi.

Alisema watu milioni 10 nchini ni maskini, idadi ambayo ni kubwa kulinganishwa na nchi nyingi barani Afrika.

Alisema idadi hiyo inatokana na kutoshiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, biashara na faida ndogo katika sekta ya kilimo ambayo ndiyo muhimili wa watu wengi wanaishi vijijni.

Alifafanua kuwa kati ya watu milioni 10 ambao ni maskini nchini, 800,000 ni vijana na kwamba wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka na ni vijana 200,000 pekee wanaobahatika kupata ajira katika sekta rasmi.

KAMATI YA BAJETI
Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Bunge ya Bajeti, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Ghasia, alisema katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mpango huo aliipongeza serikali kwa kuandaa mpango huo, huku akiitaka kuwa makini katika kutumia fedha zinazokopwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Wakichangia Mpango huo, Mbunge wa Vwawa Japhet Hasunga (CCM), alisema ili mpango huo uweze kuwa na matunda kwa jamii, lazima sekta muhimu zipewe kipaumbele.

Alisema ni wajibu wa serikali kuwekeza katika kilimo chenye tija na kuhakikisha kuwa wataalamu wa kutosha wanakuwapo ili wasaidie sekta hiyo.

Mbunge wa Liwale, Zubeir Kuchauka (CUF), alisema katika wilaya hiyo wapo, ofisa afya watatu huku mahitaji yakiwa ni 40 hali ambayo inachangiwa na kutokuwepo kwa mazingira rafiki kwa watumishi wa umma aliitaka serikali ihakikishe kuwa inalikumbuka Wilaya ya Liwale kwani imesahaulika kwa miaka mingi.

Naye Mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwako (CCM), alisema ni jambo la kushangaza kwa kuona serikali inatoa fedha za utafiti kwa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costec), wakati vipo vyuo vingi ambavyo vinafanya kazi za tafiti za kilimo lakini havina fedha.

Imeandikwa na Augusta Njoji na Sanula Athanas (Dodoma)

Habari Kubwa