Mpasuko Chadema kisa ubunge

14Jul 2020
Enock Charles
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mpasuko Chadema kisa ubunge

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepata pigo baada ya baadhi ya wanachama wake akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Ubungo, Renatus Pamba na kuhamia ACT-Wazalendo kwa kile walichodai ni ukiukwaji wa  Katiba ya Chama hicho baada ya kuwavua uongozi.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya wanachama wenzake waliohama ,Mwenyekiti huyo amesema kuwa Uongozi wa Kanda ya Pwani haukufuata katiba kwa kutangaza kuwavua uongozi bila kuwapa nafasi ya kuwasikiliza na kwamba umelenga kumependelea mgombea mmojawapo wa ubunge katika jimbo la ubungo.

“Mimi Renatus Pamba nilitia nia kugombea ubunge jimbo la Ubungo na baada ya kuonyesha nia hiyo figisu zikaanza za kuvunjwa uongozi niliokuwa nauongoza mimi Kamati ya Utendaji ya jimbo” amesema Pamba

Naye aliyekuwa Katibu Mwenezi wa jimbo hilo ,Alex Sebastian amedai kuwa kitendo cha kuvunjwa kwa uongozi wa jimbo hilo saa saba za usiku na uchaguzi wa viongozi hao kufanyika asubuhi  ni ishara ya wazi ya kutokufutwa kwa misingi ya kidemokrasia ya chama hicho na kwamba ni kwa malengom maalum ya mtia nia mmoja wapo wa ubunge katika jimbo hilo kuweka safu yake.

“Tunatambua kuwa uongozi wa Kanda unaweza kuwa na mamlaka zote za kuvunja uongozi lakini ni lazima kufuata katiba “ amesema Sebastian

“Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Pwani na Katibu wa Kanda ndugu Hemed Ally pengine hawaifahamu vizuri Katiba” ameongeza.

Baadhi ya watia nia katika jimbo la ubungo walioomba ridhaa ya chama hicho kuwania ubunge ni pamoja na aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Said Kubenea na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya ubungo Boniface Jacob.

Habari Kubwa