Mpina amshukia Tizeba bungeni

23May 2019
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Mpina amshukia Tizeba bungeni

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, ameshukia bungeni Waziri wa zamani wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, kwa kuingilia utendaji wa maofisa wa wizara yake.

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina,.

Vilevile, waziri huyo ameliomba Bunge kuipa muda serikali kuangalia kama kuna haja ya kufuta tozo ya Dola za Marekani 0.4 kwa kila kilo ya samaki wanaovuliwa bahari kuu.

Mpina aliyasema hayo bungeni jana jioni alipokuwa anahitimisha hoja ya makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha.

Alisema serikali ya awamu ya tano hakuna namna inavyoweza kumwonea mtu kwa kuwa sheria zote ambazo inazitekeleza zimetungwa na Bunge.Alisema wakati mwingine hata wabunge hugeukana anapokamatwa mtu waliye na uhusiano naye wa karibu.

"Amezungumza hapa Mheshimiwa Tizeba, Tizeba alikuwa Waziri wa (Kilimo), Mifugo na Uvuvi, lakini hata hili la kuzungumza kuwa vijana wanawaonea watu wake siyo kweli," alisema.

Mpina aliongeza: "Mheshimiwa Tizeba amekuwa akiwapigia simu vijana wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi 'kuwa-harass' na kuwaambia akiwa waziri hataki watu wake wakamatwe kwa uvuvi haramu."

Waziri Mpina alilieleza Bunge kuwa Dk. Tizeba pia amekuwa akiingilia utendaji wa watumishi wa wizara hiyo hata sasa akiwa mbunge kwamba hataki mtu wake akamatwe.

"Sasa ukifika hapa (bungeni) unabadilika kwa sababu hawa vijana hawako ndani ya Bunge, hili unawashutumu kwa kiwango hicho, siyo vizuri. Vijana wetu wanafanya kazi vizuri sana lakini kama wakifanya vibaya, tuletee tutawashughulikia tu," alisema.Kuhusu hoja ya baadhi ya wabunge kutaka serikali ifute tozo ya Dola 0.4 kwa kila kilo ya samaki wanaovuliwa bahari kuu, Mpina alisema kuna haja serikali ipate muda wa kuliangalia kwa kina suala hilo kabla ya kufikia uamuzi huo.Mpina aliwataka wabunge kuitendea haki nchi kwa sababu jambo hilo limeanzia ndani ya Bunge.“Watu walikuja na meli zenye ukubwa wa hadi tani 300, wanalipa leseni ya Dola za Marekani 65,000 (Sh. milioni 150) pekee yake.

Mbona hamjajiuliza tena samaki akivuliwa hapa anauzwa shilingi ngapi hadi waseme kuwa tuiondoe hiyo Dola 0.4?" Mpina alihoji.Waziri huyo alisema Bunge ndiyo liliiambia serikali kuwa nchi imechoka kudhulumiwa na kuonewa na meli za uvuvi zinazotoka nje ya nchi.

Alisema baada ya kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano, ilitekeleza kwa kubadili kanuni mwaka 2016 kwa kuweka mrabaha wa Dola za Marekani 0.4.“Waziri aliyekuwapo, Mheshimiwa Tizeba, alitoa 'holiday' ya miezi sita wasilipe Dola 0.4, alipotoa likizo ya Dola 0.4, Kamati ya Bunge ikabaini dosari na Tanzania imepoteza Sh. bilioni tano kwa 'holiday' ile.Mpina aliendelea kuhitimisha hoja akisema: "Waziri aliyekuwapo, aliweka kanuni na jana (juzi) aligeuka kuwa mlalamikaji ya kwamba mimi 'nime- frastuate' (nimevuruga) kwa 0.4.

Wakati wa mjadala huo juzi, Dk. Tizeba ambaye piaMbunge wa Buchosa (CCM), alisema uvuvi umekuwa kizunguzungu na kwamba yeye alifanya marekebisho makubwa ya kanuni.

Hata hivyo, Dk. Tizeba alisema baadhi yametekelezwa, lakini marekebisho katika Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu ambayo yana mwaka mmoja, bado haijaingiza fedha.

“Tumetunga sheria na kanuni ili ituongezee mapato ama ipoteze mapato? Naiomba serikali jambo hili lifanyiwe tafakari," alisema.

Habari Kubwa