Mpina awashukia anaodai wanataka kumhamisha JPM

23Jul 2019
Na Mwandishi Wetu
Simiyu
Nipashe
Mpina awashukia anaodai wanataka kumhamisha JPM

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, amewashukia baadhi ya watu waliowahi kupewa nyadhifa za juu serikalini na kwenye Chama cha Mapinduzi (CCM) kuendesha mikakati na njama za kutaka kumkwamisha Rais John Magufuli -

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina.

-kwenye ajenda kuu ya kuwahudumia wananchi na kutaka taifa lijadili mambo ya watu binafsi. 

Mpina ambaye pia ni Mbunge wa Kisesa (CCM) Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu, alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi wa jimbo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Malwilo Kata ya Tindabuligi.

Mpina alisema Watanzania wana imani kubwa na Serikali ya awamu ya tano, na kwamba mikakati na njama hizo kamwe hazitafanikiwa.

Mpina alisema viongozi hao waliwahi kupewa nafasi za juu ndani ya CCM na Serikali, lakini Watanzania walishuhudia usimamizi dhaifu wa shughuli za chama na kusababisha makundi makubwa ya viongozi na wanachama kuhamia vyama vya upinzani na kuisababishia CCM na Serikali kuchukiwa na wananchi.

Mpina alisema baada ya Rais Magufuli kufanikiwa kusuka upya mifumo, kufumua mikataba na sheria mbalimbali na kuongeza udhibiti na usimamizi wa rasilimali za nchi pamoja na kupambana na rushwa kwa vitendo na kukomesha mambo machafu yaliyokuwa yanaumiza wananchi, ndipo wanaibuka watu wachache kutoa waraka na kutaka kuwahamisha wananchi kwenye ajenda kuu ya maendeleo ili wajadili mambo binafsi kwa maslahi yao.

“Walanguzi na wala rushwa waliokuwa wanaiba fedha za taifa hili wamedhibitiwa, mishahara hewa ililipwa miaka nenda rudi viongozi wakawa wanaiba mishahara hewa kana kwamba hakuna mtu aliyetakiwa kuchukua hatua… leo Mheshimiwa John Magufuli amekuja, mishahara hewa yote imekuwa historia,” alisema Mpina.

Pia alisema Rais Magufuli amerekebisha mifumo kwenye maeneo mbalimbali ikiwamo sekta ya madini, hali iliyowezesha Serikali kuwa na hisa kwenye migodi hiyo, ambapo sasa Serikali inapata mabilioni ya fedha kutoka kwenye madini, rasilimali zetu zilikuwa zinaibwa kana kwamba hakuwapo mtu wa kuchukua hatua.

“Uvuvi haramu kila kona, samaki walikuwa hakuna Taifa lenye maziwa makubwa kuliko nchi yoyote Afrika na Dunia, Taifa lenye bahari samaki tunanunua za kutoka nje,” alisema na kuongeza:

“Mheshimiwa Magufuli akasema uvuvi haramu hapana, Mpina nenda pale kakomeshe uvuvi haramu, uvuvi haramu umekoma nchi hii, wananchi wanakula samaki wengi na wakubwa kila sehemu na mauzo ya nje yameongeka.”

Mpina alisema mambo mengine makubwa yaliyosimamiwa na Rais Magufuli kudhibiti utoroshaji fedha nje ya nchi, biashara ya dawa za kulevya, matumizi ya pombe za viroba, utoroshaji magogo nje ya nchi, uingizaji holela wa bidhaa toka nje na kuua viwanda vya ndani. Pia mikopo ya serikali, matumizi holela ya fedha za umma yote yameshughulikiwa na Serikali ya awamu ya tano.

“Sasa wengine wanaanza kujitokeza na mawaraka yao wataendelea kuyasoma wenyewe, Watanzania wako bize na maendeleo hawahitaji waraka hatuhitaji waraka sisi, tunahitaji umeme wa uhakika, sisi tunahitaji elimu bora na maji, sisi tunahitaji soko na bei nzuri ya pamba, sisi tunahitaji malisho ya mifugo, sisi tunahitaji usafirishaji wa uhakika treni, ndege, barabara, madaraja na viwanda.

Sisi tunahitaji hospitali nzuri, tunahitaji dhuluma zote dhidi ya wananchi zikomeshwe, mambo hayo Magufuli amekuwa akishughulika nayo kufa na kupona.. sisi hatuhitaji waraka…waraka wakasome wao na familia zao.”

Alisema mageuzi makubwa aliyoyafanya Rais Magufuli katika kipindi kifupi cha uongozi wake Tanzania haitamsahau na wana-CCM hawatamsahau kwa juhudi kubwa alizofanya za kuweka mifumo imara ndani ya Serikali na CCM.

“Kama ni kwenye chama nani katika historia ya nchi yetu aliyeweza kufanya kama Mheshimiwa Magufuli, nani katika utawala ambaye ameweza kurudisha wabunge 10, madiwani 200 na halmashauri nne kutoka upinzani na kujiunga na CCM?” alihoji.