Mradi wa Slale wapunguza mimba za utotoni

21Sep 2021
Zanura Mollel
Arusha
Nipashe
Mradi wa Slale wapunguza mimba za utotoni

UTAFITI umebaini kupungua kwa mimba za utotoni kwenye maeneo yanayotekeleza mradi wa kuzijengea asasi uwezo kwenye masuala ya afya ya uzazi kwa vijana (Slale) unaotekelezwa kwa zaidi ya mikoa mitano hapa nchini.

Hayo yamebainishwa kwenye mkutano wa kufanya tathmini ya mradi huo uliofika ukingoni jijini Arusha na mratibu wa mafunzo kwa vijana nchini Fausta Kambanga.

Akiwasilisha tathmini ya mradi huo katika Manispaa ya Kinondoni ambapo mradi huo ulikuwa unatekelezwa kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Kambanga amesema mwaka 2015 kabla ya mradi kuanza mimba za utotoni zilikuwa 14% lakini mwakaja 2020 zimepungua hadi 7%.

"Tunapozungumzia mimba za utotoni ni wale wanaopata mimba chini ya miaka 20 ambapo mwaka 2015 idadi ya waliopata mimba katika Manispaa hiyo kwa ujumla walikuwa 35785 huku mimba za utotoni zikiwa 5010 na kwa mwaka 2020 jumla walikuwa 36703 huku mimba za utotoni zikiwa 2617" amesema Kambanga.

Kwa Halmashauri ya Arusha (Arusha DC) ambapo mradi ulikuwa ukitekelezwa tathmini imeonyesha ongezeko la matumizi ya uzazi wa mpango kwa vijana jambo linalochochea kupungua kwa mimba za utotoni.

Mratibu huduma ya afya ya uzazi na mtoto katika halmashauri hiyo Butolwa Bujiku, amesema kwa kipindi cha Julai - Desemba 2020 kati ya waliopata huduma ya uzazi wa mpango kwa njia ya vipandikizi ni 11270, vijana walikuwa 3782 ambao ni sawa na 33% ya vipandikizi vyote vilivyotolewa.

"Matumizi ya uzazi wa mpango kwa vijana yamekuwa yakiongezeka, ukiachilia mbali vipandikizi, Kondomu zinafuata kwa ongezeko ambapo zimefika 30% mwezi Januari-Juni mwaka huu wakati Julai-Desemba mwakajana ilikuwa 28% ya watu wote waliotumia njia hiyo" amefafanua.

Edmund Ardon afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambapo mradi huo unatekelezwa pia alisema ni wazi mimba za utotoni zimepungua kwani kwa kipindi cha Januari-Juni mwaka huu vijana waliotumia njio ya vipandikizi ni 1166 mbali na njia zingine kama vidonge, Kondomu, sindano na kitanzi.

Helen Pascal mratibu wa mradi wa SLALE (Strengthening Local Advocacy Leadership) amesema asasi ambazo wamezijengea uwezo ni DOYODO ya jijini Dodoma, HIMD ya Arusha, YWCA ya Dar Es Salaam, GRABHAH na KIVULINI za Mwanza na Tanzania Red Cross Shinyanga ambazo zimeweza kuandaa afua mbalimbali za vijana ambazo zimewawezesha kupata wafadhili nje na DSW.

Helen amesema mradi katika miaka minne ya utekelezaji wameweza kuzijengea uwezo asasi hizo kwenye masuala ya vijana hasa katika eneo la afya ya uzazi na uzazi wa mpango achilia mbali kuimarisha mahusiano ya asasi hizo na serikali, wametambua vipaumbele, sera na miongozo mbalimbali ya serikali sambamba na kurekebisha mapungufu mbalimbali ya yaliyojitokeza ikiwemo upelekaji wa ripoti za utekelezaji wa miradi katika ngazi husika.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Shirika la DSW Tanzania Peter Owaga alisema pamoja na kwamba shirika linajihusisha na maendeleo ya vijana lakini ni vigumu kuwafikia vijana kila mahali hivyo wakaona kuna haja ya kupanda mbegu ya kuzijengea uwezo asasi mbalimbali ili ziendelee kuelimisha vijana hata kama mradi utakuwa umefika tamati.

"Tuliangalia changamoto za vijana kwenye kila eneo la utekelezaji wa mradi mfano kuna maeneo ambayo maambukizi ya VVU yalikuwa juu, mengine mimba za utotoni hivyo mbali na kutoa elimu ya pamoja lakini pia kila asasi ilipata mafunzo ya peke yake kulingana na mahitaji ya eneo husika" ameongeza.

Hata hivyo meneja miradi wa shirika hilo Philomena Marijani, ameeleza matarajio yake kuwa pamoja na kwamba mradi umefika ukingoni ni wazi yale yote yanayohusiana na kumwendeleza kijana yataendelezwa kama ambavyo dira yao ni kumjengea kijana mazingira wezeshi katika masuala ya kiuchumi, kutambua kipaji chake, afya na afya ya uzazi.