Mradi wa bil. 116/- kumaliza tatizo la maji Dar, Pwani

19Dec 2018
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Mradi wa bil. 116/- kumaliza tatizo la maji Dar, Pwani

TATIZO la maji katika Jiji la Dar es Salaam na Pwani linatarajia kubaki historia baada ya ujio wa mradi mkubwa wa kusambaza maji unaotarajia kugharimu Sh. bilioni 116.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, picha mtandao

Mradi huo utasambaza maji katika jiji lote la Dar es Salaam yakiwamo maeneo yenye tatizo sugu la maji ya Goba, Kimara pamoja Mkoa wa Pwani.

Mbali na mradi huo, serikali kupitia Wizara ya Maji, imejenga tangi lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 180 za maji ambalo litasaidia kusambaza katika eneo lote la Wilaya ya Bagamoyo na maeneo jirani na viwanda mkoani Pwani.

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa, alithibitisha kumalizika kwa tatizo la maji katika Jiji la Dar es Salaam na Pwani katika ziara yake jana ya kusikiliza, kutatua kero za maji na kutembelea miradi mbalimbali katika Wilaya ya Bagamoyo.

Akizungumzia mradi wa maji wa Sh. bilioni 116, Profesa Mbarawa alisema tayari pesa hiyo imepatikana na wapo katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi.

Alisema serikali inafahamu tatizo kubwa la maji lililopo katika Jiji la Dar es Salaam na kwamba tayari imeanzisha miradi mbalimbali ya kumaliza kabisa tatizo hilo kufikia mwaka 2020.

"Tunafahamu tatizo kubwa la maji lililopo katika Jiji la Dar es Salaam, na yapo maeneo ambayo hayajawahi kupata kabisa maji ya bomba, ninataka niwahakikishie kwamba tatizo la maji sasa litabaki kuwa historia, haijalishi ni vijijini au mjini, maeneo ya milima na yasiyo ya milima," alisema Profesa Mbarawa na kuongeza:

"Tayari pesa ipo na lengo letu ifikapo 2020 tuwe tumefikisha asilimia 95 ya wananchi wanaopata huduma ya majisafi na salama, naomba niwahakikishie Watanzania kwamba watapata maji wote kwa sababu serikali imekuja na mpango wa kuchukua maji kutoka kwenye vyanzo vya maji na kuyafikisha sehemu ya makazi ya wananchi."

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Bagamoyo (Dawasa), Alex Ng'wandu, alisema mpaka sasa wanaopata majisafi na salama Bagamoyo ni 5,900 na wanatarajia kuongeza wateja zaidi.

Habari Kubwa