Mradi waja kukabili athari  za mabadiliko ya  tabianchi

29Nov 2021
Na Mwandishi Wetu
NAIROBI, KENYA
Nipashe
Mradi waja kukabili athari  za mabadiliko ya  tabianchi

KATIKA juhudi za kusaidia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kampuni ya Qnet imezindua mradi wa upandaji miti uitwao ‘Urithi wa Kijani’, unaolenga kuhamasisha upandaji na utunzaji wa miti barani Afrika.

Kupitia mradi huu, shirika hilo limepanda zaidi ya miti 3,000 barani Afrika na Asia.  Kenya, mradi huu unatekelezwa katika maeneo ya vijijini chini ya ushirikiano na kikundi kiitwacho Trees4Kenya.

“Kwa kushirikiana na Trees4Kenya, tunajitahidi kubadilisha kiwango cha kaboni cha Kenya na tuna nia ya kujenga jumuiya endelevu kote barani Afrika,” alisema Mratibu wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Qnet, Muqtadir Suwani.

Suwani alikuwa akizungumza hivi majuzi nchini Kenya wakati wawakilishi wa kampuni hiyo walipotembelea maeneo ya upandaji miti huko Embu, Kenya.

"Hakuna wakati kama wa sasa wa kuwa rafiki na mazingira...Qnet inaunga mkono jitihada za serikali kutunza mazingira na kuleta mabadiliko chanya," aliongeza.

Suwani aliendelea kuelezea mradi huo kama ushirikiano wa wadau mbalimbali unaofanya kazi katika ngazi ya jamii kupitia ushirikiano na wadau kama vile EcoMatcher na kikundi cha Trees4Kenya.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Trees4Kenya, Paulino Mugendi, alisema ushirikiano huo wa sekta binafsi ni muhimu ili kuokoa misitu ya Kenya.

“Tunashukuru sana Qnet na washirika wao kwa msaada huu…ni kwa kupanda miti tu ndipo tunaweza kulinda mazingira yetu vyema,” alisema mwanamazingira huyo.

 “Tayari tumepanda mamia ya miti na kupitia mradi huu tunatarajia kupanda zaidi ya miti 1000 na kwa njia hiyo kusaidia kurejesha misitu nchini Kenya,” aliongeza.

Pia alikuwapo Karuku Kathogo, mtaalamu wa misitu kutoka Forestry Kenya ambaye alisema zaidi ya kulinda mazingira, kupanda miti pia kunasaidia maendeleo endelevu ya jamii.

"Mipango hii inahakikisha kwamba tunakuwa na jumuiya endelevu ambayo haiharibu mazingira yake kwa jina la maendeleo," alisema.

Marehemu Wangari Mathai, mwanzilishi wa Green Belt Movement nchini Kenya aliwahi kusema, “…watu maskini watakata mti wa mwisho ili kupika mlo wa mwisho.”

Mwanamazingira alisema maneno hayo akimaanisha jitihada za utunzaji mazingira lazima ziende ana kwa ana na utokomezaji wa umaskini. Mathai alihamasisha upandaji wa zaidi ya miti milioni 30, na kuhamasisha Umoja wa Mataifa kuanzisha kampeni ambayo imesababisha kupanda miti bilioni 11 duniani kote.

Hata hivyo, kwa vile umaskini unazidi kushamiri, Afŕika sasa inapoteza misitu mingi kila siku na jambo la kusikitisha ambalo lilifichuliwa katika mkutano wa COP26 mwaka huu ni kwamba Afŕika bado haipewi ufadhili unaohitajika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Habari Kubwa