Mrema atua polisi kudai fidia bil. 20/-

13Jan 2018
Beatrice Shayo
Nipashe
Mrema atua polisi kudai fidia bil. 20/-

MWENYEKITI wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema, amefungua kesi ya kutaka alipwe Sh. bilioni 20 kwa kitendo cha kuzushiwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa amefariki dunia.

MWENYEKITI wa Taifa wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam baada ya kutoka kufungua kesi katika kituo cha polisi cha Oysterbay, Mrema alisema alikwenda kutoa taarifa kwenye Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) na kumtaka aende kituo cha polisi ili apatiwe RB.

“RB yangu ni OB/RB/613/2018 kuhusiana na matumizi mabaya ya mtandao. Nadai fidia ya Sh. bilioni 20 na haitapungua hata mia ili kuwashikisha adabu na tayari polisi wameniambia kazi itaanza leo (jana),” alisema Mrema.

Aidha, Mrema alisema analalamikia mambo mawili kuwa Januari 9, mwaka huu, kupitia mitandao ya kijamii, ilidaiwa kuwa amefariki dunia jambo ambalo lilimsababishia usumbufu.

“Lengo lao walitaka kuharibu kazi yangu ambayo nilikuwa naenda kuifanya kule Kiraracha (kijijini kwao mkoani Kilamanjaro). Hiyo siku nilikuwa nimepanga kwenda kujenga makaburi ya baba yangu, mama na mdogo wangu ambao walishafariki dunia,” alisema.

Aliongeza kuwa: “Ilikuwa siku ambayo tungekutana watu wengi huko Kiraracha kwa kuwa ni sehemu niliyozaliwa na pia siku hiyo nilipanga  kusoma misa ya kuwaombea ndugu zangu waliofariki (dunia) pamoja na kumshukuru Mungu maana nilikuwa mgonjwa na kwa sasa nimepata nafuu.”

Mrema alisema kutokana na taarifa hizo kwenye mitandao, walimvurugia kufanya kazi na ndugu zake badala ya kwenda kwenye tukio lililopangwa (kujengea makaburi), walianza kuomboleza.

Kutokana na hali hiyo, Mrema ambaye amewahi kutumikia nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwamo ya Naibu

Waziri Mkuu, alisema familia yake ilikumbwa na simanzi hasa watoto wake, ndugu zake na wafuasi wake kwa kumzushia kifo.

“Nilipigiwa simu nyingi sana na wengi walilia na kusikitika kutokana na taarifa hizo za (uzushi za) kifo changu,” alisema 

Aidha, alisema jambo la pili ambalo ameliona ni kutaka kuvuruga mkutano wa Rais John Mafuli na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kwa sababu Januari 9, mwaka huu, Rais alipanga kufanya mkutano wake Ikulu na Lowassa.

“Kwa hiyo wakajua kuwa Rais atapata ‘kiki’ atafanikiwa katika mambo yake na wapinzani wake wamezoea kutukana hasa katika mitandao na kumpiga vita.

Sasa  nimeelewa kwa nini wanataka kupiga vita vyombo vya habari vinataka kutumika kuwachafua watu kama ilivyonitokea mimi ili Rais asifanikiwe mkutano wake na Lowassa wakaamua kuzusha kifo cha Mrema. 

“Si mnajua Mrema ni mtu mashuhuri anayejulikana kwa hiyo ukisema Mrema amekufa hakuna mtu ambaye atakuwa makini kwa Lowassa na Rais,” alisema.

Alisema jambo hilo ni la hatari na linatakiwa kuzuiwa kwa gharama zozote  na endapo mitandao itatumika kwa aina hiyo (kuwachafua au kuwazushia watu), haitakuwa na maana. 

Habari Kubwa