Mrindoko ataka maelezo idadi ya majengo vituo vya afya Katavi

14Oct 2021
Neema Hussein
Katavi
Nipashe
Mrindoko ataka maelezo idadi ya majengo vituo vya afya Katavi

MKUU wa mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amemtaka mganga mkuu wa mkoa kufika ofisini kwake na kutoa maelezo kuhusu idadi ya majengo ya vituo vya afya vinavyojengwa katika manispaa ya Mpanda.

Mrindoko amefikia uamuzi huo kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa kituo cha afya cha Kakese kilicho katika manispaa ya Mpanda.

Amesema wizara imetoa kiasi cha Mil. 500/- fedha na imeelekeza kujenga majengo tisa katika kituo hicho, lakini taarifa aliyosomewa ikionyesha ni majengo matano tu yaliyokamilika.

"Lazima ijulikane mnajenga majengo mangapi na mkubaliane kwa maandishi siyo mnajenga alafu mkifika katikati mnasema tuongeze tena jengo moja hapo mnatengeneza upotevu wa pesa za serikali," amesema.

Amesema maelezo alioyapata yanasema mganga mkuu wa manispaa na mhandisi walikubaliana na mganga mkuu wa mkoa kuwa wajenge matano, huku akihoji wizara ndio iliwaambia hivyo wakifika huko waanze kushauriana.

Hata hivyo, Mrindoko amesema hajafurahishwa na kitendo cha kuchelewa kuanza kwa ujenzi wa kituo hicho, huku akisema fedha imetolewa Juni 3, 2021 na ujenzi umeanza Septemba mwaka huu.

Amesema kituo hicho ni muhimu sana na kinategemewa na wakazi wa kata ya kakese na maeneo jirani, huku akisisitiza kufanya hivyo ni kuendelea kuwachelewesha wananchi hao kupata huduma za afya.

Habari Kubwa