Msaidizi wa Membe ajisalimisha polisi Dar

10Jul 2019
Romana Mallya
Dar es salaam
Nipashe
Msaidizi wa Membe ajisalimisha polisi Dar

ALLAN Kiluvya, msaidizi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana siku tatu zilizopita, hatimaye amepatikana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Musa Taibu-

-ameiambia Nipashe jana kuwa, Allan alikwenda polisi juzi usiku na kuwaeleza kuwa alikuwa ametekwa na watu wasiojulikana na kumuachia huru.

"Allan aliyetekwa amepatikana, alikuja mwenyewe polisi jana (juzi) usiku na akasema kuwa alitekwa na watu ambao mpaka wakati huo hajawafahamu kwa sababu wakati wakimchukua walimfunga kitambaa usoni na hata huko alipopelekwa hakujui," alisema.

Kamanda Taibu alisema ingawa bado hajaonana uso kwa uso na Allan, ameambiwa kuwa alipofika kituoni alieleza kuwa amekwenda hapo kutoa taarifa kuwa amepatikana.

"Sijaongea naye kwa sababu leo tangu asubuhi sipo ofisini. Nimeambiwa kuwa Allan amesema aliwekwa katika mazingira ambayo hakuyapenda, sababu za kutekwa hajui, hakuna manyanyaso waliyompatia.

Jeshi la Polisi litamuhoji Allan kujua zaidi baada ya kutekwa, hao watekaji walimwambia nini, lengo lao lilikuwa ni lipi? Tunamtaka achukue tahadhari kwa sasa, wakati tukipanga kumuhoji zaidi kuhusu tukio hilo," alisema.

Awali, mjomba wa kijana huyo, Samwel Ng'andu, akizungumza na waandishi wa habari alisema jaribio la kutekwa Allan lilianzia baa ya Rose Garden iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.

"Jaribio la kutekwa lilianzia Rose Garden, idadi ya watekaji ilikuwa ni watu wanne walikuwa wakitumia gari aina ya Land Cruiser T810 BQS, rangi ya kijivu na lilikuwa na gurudumu nyuma lililofunikwa kwa kava lenye rangi ya chungwa," alisema.

Aliongeza: "Baada ya tukio hilo kushindikana kijana wetu aliendelea kufanya mizunguko kwa uangalifu hadi siku alipotekwa na gari lile lile la Land Cruiser," alisema.

Jumatatu, Kamanda Taibu aliwaomba mwananchi wenye taarifa mahali alipo, wawasiliane na Jeshi la Polisi kwa sababu hadi siku hiyo walikuwa hawajampata.

"Taarifa tayari tumezipata tunaendelea kuzifanyia kazi, lakini tunaomba hata wewe mwandishi kama una taarifa au fununu wapi alipo utusaidie, kama kuna mwananchi ana taarifa alipo wawasiliane nasi. Lengo ni ili apatikane," alisema.

Jumapili, kulizagaa taarifa mitandaoni ikidai Allan alitekwa na watu wasiojulikana maeneo ya Mbezi Jogoo, jijini Dar es Salaam nje ya nyumba ya rafiki wake.

Katika maelezo yake, Magreth aliyojirekodi kuhusiana na tukio hilo la utekaji alidai kuwa, siku ya tukio walikuwa hoteli ya Mbezi Africana yeye, dada yake Agnes pamoja na Allan na baada ya kunywa, kijana huyo aliwapeleka nyumbani kwao Jogoo.

"Nilikuwa mimi, Allan na dada yangu mwingine anaitwa Agnes, tulikuwa hoteli ya Juliana kule Africana, baada ya kunywa ulifika muda wa kwenda nyumbani, Allan akasema atatupeleka, siyo mbali na hapo Juliana, ni Jogoo kituo kinachofuata. Alitupeleka hadi nyumbani, nikashuka na kufungua geti akaingiza gari akashuka Allan na dada yangu," alisema.

Magreth aliendelea kusimulia: "Allan alitaka kumsalimia mama yake ambaye wakati huo alikuwa hajalala, alimsalimia wakaongea muda wa kuondoka aliniambia nimfungulie geti ili atoke, nilifungua na kulifunga, nilikuwa nimemuomba fedha, si unajua ile kikaka kaka aniachie pocket money (fedha za matumizi) kidogo, akaniambia niende nje tuongee. Akarudi kinyume nyume, nikafunga geti, nikatoka nje.

Nilipotoka nikasogelea gari lake kwa mbele ambako Allan alikuwa anaelekea kulikuwa na gari iliyokuwa ikipandisha kwa sababu kuna kibonde, ilikuwa inaelekea upande wa kulia alikokuwa Allan."

Vile vile aliendelea kusimulia kuwa, baada ya gari hiyo kupita, ilikuja nyingine aina ya Land Cruiser ikitokea nyuma ya gari la Allan.

"Hiyo Land Cruiser ilikuwa na rangi kama ya khaki, brown au gold hivi, nikamwambia Allan kuwa kuna gari nyingine nyuma ili asogee mbele aipishe, Allan aliniambia mbona njia ni kubwa sana, nikamwambia asogee ili kuepusha ugomvi, akasogea, aliposogea kama anarudi getini ile gari nayo ikasogea, nikamwambia asogee tena ili kuepusha ugomvi, aliposogeza gari alishuka na yule mtu kwenye Land Crusier naye akashuka," anasimulia.

Magreth alieleza kuwa, baada ya dereva wa gari la Land Cruiser kushuka aliangalia mbele na nyuma na akawauliza kwani vipi.

"Allan naye alimuuliza kwani vipi, na mimi nilimuuliza mbona tumekupisha hujapita, wakati namalizia kujibu nilipomgeukia Allan, nikaona watu wamezunguka gari, wawili pembeni yetu, wawili nyuma yangu na wengine walikuwa kama saba na yule kaka wa kwanza.

Wakamvamia Allan na kumpiga, Allan alikuwa anasema Mage nisaidie, yule kaka wa kwanza akaninyooshea bastola, nikasikia mmoja anasema mchukue na huyo (yaani mimi), huyu hakutii alichoambiwa na mwenzake, akaniambia nifanye haraka niingie ndani, nikanyata kurudi ndani sikufunga geti na komeo, nilipofika mlango wa kuingia ndani ya nyumba nikapiga kelele Allan ametekwa."

Magreth anadai kuwa, walipotoka walikuta wameshaondoka ingawa kuna watu wa bodaboda walijitokeza na kueleza kuwa gari hilo lilipita mtaani hapo kama mara tatu.

"Tukio hili lilichukua kama dakika tatu hivi. Ila wakati tunatoka baa kuna bodaboda niliiona kama vile ilikuwa inatufuatilia, lakini sikuitilia maanani, hawajachukua kitu waliacha gari, funguo, simu yake smart phone, simu yake ndogo ambayo alikuwa nayo ambayo ni ya laini yake ya Tigo, hata polisi tumejaribu kuipiga kaipatikani," Magreth alidai.

Tukio hili ni la pili baada ya la Juni 24, la mfanyabiashara Raphael Ongangi, raia wa Kenya aliyedaiwa kutekwa maeneo ya Oysterbay, jijini Dar es Salaam na watu wenye silaha akiwa na mke wake, Veronica Kundya na kupatikana Jumanne iliyopita huko Mombasa.

Habari Kubwa