Msako mkali waliochepusha maji

15Jan 2022
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Msako mkali waliochepusha maji

SERIKALI wilayani Morogoro imeziagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MOROWASA) na Bonde la Wami/Ruvu kufanya operesheni maalumu ukuwasaka watu waliochepusha maji katika mito inayongiza maji katika Bwawa la Mindu.

Watu wamechepusha maji katika vyanzo vya mito hiyo kwa ajili ya shughuli za kibinadamu, hivyo kusababisha upungufu wa maji katika bwawa hilo. Mito hiyo ni Mzinga, Ngerengere, Mgeta na Mlali.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Albert Msando, alitoa agizo hilo jana baada ya kufanya ziara ya siku mbili katika mito na vyanzo vya maji na kushuhudia baadhi ya watu wakiwa wamechepusha maji kwenye mito hiyo kwa ajili ya shughuli za kilimo.

“Agizo la serikali nendeni mkafanye operesheni ya kuondoa watu waliochepusha maji kwenye mito yote ambayo ni chanzo cha maji katika Bwawa la Mindu. Asije kutokea mtu anasema eti kumwagilia shamba au nyanya ni bora, kafanyeni shughuli kuokoa wana Morogoro.  Sharia ipo kamateni, pelekeni Mahakamani mara moja,” alisema Msando.

Mkuu huyo wa wilaya alisema wakazi wa Manispaa ya Morogoro wanalitegemea Bwawa la Mindu kwa asilimia 70 kwa ajili ya kupata maji, hivyo uharibifu unaofanyika wa kuchepusha maji endapo utachwa, kuna hatari siku zijazo wananchi hao wakakosa maji.

Msando alisema pamoja na kuwapo kwa ukame katika kipindi hiki, mvua zinapoanza kunyesha ni lazima sasa kila nyumba ipande miti miwili pamoja na wananchi  kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kupanda miti katika maeneo ya vyanzo vya maji.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Morowasa, Mhandisi Tamimu Katakweba, alisema uharibifu wa mazingira, kuingiza mifugo na uchepushaji wa maji katika vyanzo vya maji ni moja ya sababu za kukauka kwa mito ambayo ndiyo tegemeo la kuingiza maji katika Bwawa la Mindu.

Alisema kwa sasa MOROWASA inatekeleza miradi mikubwa yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 13 pamoja na kujenga miundombinu mbalimbali ya kusambaza maji katika Manispaa ya Morogoro.

Katakweba alisema endapo uharibifu wa mito hiyo utaendelea, miradi hiyo itakuwa haina maana yoyote na wakazi hao wataendelea kukosa huduma ya maji.

Mhandisi wa Rasilimali za Maji kutoka Bonde la Wami/Ruvu, John Kassambili, alisema wataanza mara moja operesheni hiyo kuwakamata wale wote waliochepusha maji katika mito yote katika mkoa wa Morogoro na kuwataka wananchi kuwapa taariza kwa watu wanaofanya hivyo.

Habari Kubwa