Msako wa madalali ‘vishoka’ waanza rasmi

25Feb 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Msako wa madalali ‘vishoka’ waanza rasmi

SERIKALI imesema kuanzia sasa hakuna dalali atakayeendesha shughuli hizo bila kujisajili na kuwa na leseni.

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James (kushoto), akizungumza na wawakilishi wa madalali pamoja na wahakiki mali wa mikoa Tanzania Bara, kabla ya kuzindua Mfumo wa Kieletroniki wa Utoaji Leseni za Udalalli na Uendeshaji wa Minada ya Hadhara Tanzania Bara, jijini Dar es Salaam jana. PICHA: WFM

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James, wakati akizindua mfumo wa utoaji leseni za udalali na uendeshaji minada kwa njia ya kielektroniki, uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema tayari shughuli hizo ni rasmi na wanaotakiwa kuziendesha ni waliosajiliwa pekee na kwamba wamejipanga kuanza kufanya oparesheni katika kila mtaa maeneo mbalimbali nchini kuwakamata madalali ambao hawajajisajili

Pia alisema madalali feki wote watakaokuwa wanakamatwa kufanya shughuli hizo bila kuwa na leseni, watakuwa wanatangazwa kwenye vyombo vya habari.

"Kama unajiita ni dalalli na unafanya shughuli hizo bila kujisajili, mwisho wako umefika, serikali tuna mbinu mbalimbali za kufanya shughuli zetu, tutapita huko mitaani kwenu tutawakamata na hatutakuwa na huruma, tutakutana nao mahakamani Kisutu," alisema James.

"Wanatapeli watu kwa muda mrefu, wamesababisha hata wale waaminifu ambao wamejisajili na kulipa kodi serikalini nao waonekane ni matapeli, ilifika wakati hata kwenye familia mtu mmoja akiwa dalali, familia yote inadharaulika, sasa huu ni mwisho wao, hii sekta ni rasmi kama zilivyo nyingine,"

Katika uzinduzi huo, Katibu Mkuu huyo alisema usajili kwa sasa umerahisishwa na kwamba watajisajili kwa njia ya mtandao kupitia komputa au simu za mkononi katika mikoa wanayoishi badala ya kusafiri mpaka Dodoma kama ilivyokuwa zamani

"Mfumo huu utasaidia kufahamu taarifa sahihi za madalali na pia kufahamu na kuwabaini kwa urahisi wanaofanya shughuli hizo bila kujisajili,"alisema James

Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mali za serikali kutoka Wizara hiyo, Choto Sendo, alisema idadi ya madalali wanaotakiwa kujisajili ni wote wanaofanya shughuli hizo ikiwamo wanaoendesha minada ya hadhara kwa Tanzania Bara, ukusanyaji wa madeni, ushuru, tozo, udalali wa mahakama, nyumba, viwanja na mwingineo unaofanana na huo

Mkurugenzi Mtendaji wa Yono Action Mart, Scholastika Kevela, aliipongeza serikali kwa kupiga mafuruku madalali feki kuwa walichangia ionekane ya kitapeli

Pia alisema kwamba wako tayari kuisaidia serikali kuwafichua madalali feki wote ili kuhakikisha hakuna anayefanya shughuli hizo bila kujisajili

Habari Kubwa