Msando, wafuasi wake Instagram wamlipia deni Rais Magufuli

23Aug 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Msando, wafuasi wake Instagram wamlipia deni Rais Magufuli

WANANCHI wamemlipia Rais John Magufuli deni la Sh. milioni 5 kati ya Sh. milioni 5.364 alizokuwa anadaiwa na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kuahidi kulipa deni la matibabu ya marehemu Sabina Loita (52) alilokuwa anadaiwa mtoto wake.

MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa (MNH), Prof. Lawrence Museru akipokea fedha kutoka kwa niaba ya wafuasi wa ukurasa wake Instagram leo.

Agosti 11, mwaka huu, Rais Magufuli akiwa hospitalini hapo kuwajulia hali majeruhi 43 waliopata ajali ya moto mkoani Morogoro, alikutana na mama aliyemuomba msaada wa kulipa gharama za matibabu ya mama yake mzazi ambaye mwili wake ulizuiliwa MNH.

Rais Magufuli aliahidi kulipa deni hilo huku akiutaka uongozi wa hospitali hiyo kumpelekea yeye gharama zote za matibabu hayo na kuagiza mama huyo kukabidhiwa mwili wa mzazi wake

Wakili Albart Msando, alikabidhi fedha hizo kwa niaba ya wafuasi wa ukurasa wake Instagram leo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Lawrence Museru, alisema aliamua kuchangisha fedha hizo baada ya kuvutiwa na nia ya Rais Magufuli ya kumsaidia mama huyo.

"Zipo sababu tatu zilinifanya nikaguswa kuamua kuchangisha fedha hizi za kusaidia kulipa deni la Rais Magufu moja ni ule moyo wake wa ubinadamu wa kutaka kumsaidia na akasema MNH wamdai yeye binafsi, wakati alikuwa na uwezo wa kuagiza hospitali ifute deni hilo au Serikali ilipe gharama hizo," Msando amesema.

Amesema pia wametumia fursa hiyo kuhamasisha matumizi mazuri ya mitandao ya kijamii na kuhamasisha jamii kusaidia wahitaji kwa sababu hospitali hiyo ina wagonjwa wengi wasiyo na uwezo wa kupata matibabu.

Habari Kubwa