Msekwa amthibitisha rasmi Prof Sife kuwa Makamu Mkuu wa MoCU

22Oct 2019
Godfrey Mushi
Moshi
Nipashe
Msekwa amthibitisha rasmi Prof Sife kuwa Makamu Mkuu wa MoCU

SPIKA wa zamani wa Bunge la Tanzania, Pius Msekwa amemthibitisha rasmi Prof. Alfred Said Sife kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU), baada ya kuwabwaga maprofesa wengine saba katika kinyang’anyiro hicho.

Spika wa zamani wa Bunge, Pius Msekwa akimkabidhi rasmi barua ya uteuzi Prof. Alfred Sife kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi. picha Godfrey Mushi.

Msekwa ambaye ni Mkuu wa chuo hicho, alitangaza jana uteuzi huo baada ya Prof. Sife kuwashinda wenzake katika mchakato wa kuwatafuta na kuwapima, wanataaluma wengine ambao ni maprofesa kutoka vyuo vikuu sita nchini.

“Sasa namtangaza rasmi Profesa Alfred Said Sife, kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na uteuzi wake unaanza leo (Oktoba 21, 2019).

“Mchakato wa kumtafuta ulikuwa ni shirikishi na ulihusisha wadau wote na matokeo yake mchakato huo umezaa matunda. Mchakato huu wa kumtafuta Makamu Mkuu wa Chuo ulianza rasmi Aprili 29 mwaka huu. Siku Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, George Yambesi alipounda kamati ya watalaam kubaini wanataaluma ambao wanafaa mmojawapo kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushiika Moshi.” Prof. Sife aliwabwaga katika kinyang’anyiro hicho maprofesa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Mzumbe, Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA), Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Nafasi hiyo ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi ilikuwa wazi tangu Prof. Faustine Bee, alipoteuliwa kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),

Machi mwaka huu. Aprili 2 mwaka huu, Msekwa alimteua Prof. Sife aliyekuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (Taaluma), kukiongoza chuo hicho kwa muda wote ambao watakuwa wanamtafuta mkuu wa chuo atakayeshika mikoba ya Prof. Faustine Bee.

Wakati anatangaza uteuzi huo mbele ya wanataaluma, wafanyakazi na serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Msekwa alisema: “Kamati yangu iliyokuja na majina na mapendekezo yao ya nani anastahili kuwa Makamu Mkuu wa chuo chetu cha Ushirika Moshi, ilikuwa na wajumbe watatu ambao ni wanataaluma waliobobea, Profesa Lucian Msambichaka ambaye ndiye Mwenyekiti wa kamati ile na wajumbe wake wawili ni Profesa Gerald Monela na Profesa Joseph Kuziwa.”

Kwa mujibu wa Msekwa, kamati hiyo ilikubaliana kuwatafuta wanataaluma popote pale yaani ndani na nje ya nchi, lakini ilibidi wazingatie muongozo uliotolewa katika kanuni husika na kamati hiyo ilifanikiwa kupata jumla ya wanataaluma wanane, wawili wanatoka MoCU na sita wanatoka vyuo vikuu vingine.

Habari Kubwa