Msekwa aanza kazi kwa kutunuku PhD

10Dec 2018
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Msekwa aanza kazi kwa kutunuku PhD

SPIKA wa zamani wa Bunge la Tanzania, Pius Msekwa, kwa mara ya kwanza ameandika historia ya kutunuku Shahada ya Uzamivu (PhD) watu watatu waliofuzu vigezo vya kitaaluma tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) mwaka 2014.

SPIKA wa zamani wa Bunge la Tanzania, Pius Msekwa.

 

Alifanya kazi hiyo juzi ikiwa ni siku tatu tangu Rais Dk. John Magufuli, amteue kuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST).

Msekwa sasa anakuwa mkuu wa vyuo vikuu viwili nchini, ambavyo ni Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya.

Kabla ya kutunuku shahada hizo katika mahafali ya nne yaliyofanyika mjini Moshi, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, George Yambesi, ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, alimweleza kuwa kati ya wahitimu 1,623 atakaowatunuku astashahada, stashahada, shahada za awali, stashada za uzamili na shahada za umahiri, wamo watatu waliofanikiwa kufikia vigezo vya kupewa shahada za uzamivu.

"Kati ya matunda utakayoyashuhudia leo ni pamoja na wahitimu watatu wa shahada ya uzamivu (PhD), hawa ni wahitimu wa kwanza kwa Chuo hiki Kikuu cha Ushirika Moshi.

Kuhitimu kwao ni alama tosha ya mafanikio ya kujivunia katika maisha yao, kwa kuwa inatokana na juhudi na maarifa waliyowekeza.

"Elimu waliyoipata itawasaidia kuendeleza falsafa ya uchumi wa viwanda na kuwa mabalozi wetu wazuri wa kuhakikisha azma hii ya serikali ya awamu ya tano inatimia.

Mmekuwa miongoni mwa wasomi katika taifa letu na tunategemea elimu mliyoipata itakuwa nguzo katika kutatua matatizo na kuhudumia jamii kwa uzalendo, uadilifu, utendaji mzuri na ubunifu.

Awali, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Prof. Faustine Bee, alimweleza Msekwa kuwa kati ya wahitimu 1,623, wanawake ni 753 ambao ni sawa na asilimia 46.4 na wanaume ni 870 sawa na asilimia 53.6

Profesa Bee pia alimpongeza Msekwa akisema: "Nitumie fursa hii kwa kumshukuru mheshimiwa rais wetu (Magufuli), kwa kukuona kwamba unastahili kupewa na kazi hii ya pili, baada ya kuifanya vizuri kazi ambayo unaendelea kuifanya katika chuo chetu."