Mshauri elekezi asakwa kuvuna maji

15Feb 2020
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
Mshauri elekezi asakwa kuvuna maji

BODI ya Maji Bonde la Wami/Ruvu, imetangaza zabuni ya kumpata mshauri elekezi atakayefanya utafiti jinsi ya kuvuna maji ya mvua ili kuyahifadhi katika chanzo cha maji cha Mzakwe Makutupora.

Chanzo hicho ni pekee cha maji kwa wakazi wa Dodoma, na lengo ni kuendana na ongezeko la watu katika jiji hilo.

Kauli hiyo ilitolewa na Ofisa wa Bodi ya Maji wa Bonde hilo, Simon Ngonyani, wakati akizungumza na Nipashe baada ya bodi hiyo kutembelea chanzo hicho kwa lengo la kujionea changamoto zilizopo na kuzipatia majibu kwa ajili ya kuhakikisha zinatatuliwa.

Ngonyani alisema shughuli za Serikali zote zimehamia Dodoma ambapo ni makao mkuu ya nchi, na wakazi wake wanategemea maji kutoka chini ya ardhi ambapo chanzo cha Mzakwe Makutupola ndio chanzo pekee cha maji kinachotengemewa huku matumizi ya maji yakiongezeka.

“Kwa sasa kuna zabuni ambayo tumetangaza ya kumpata mshauri elekezi afanye utafiti jinsi ya kuvuna maji ya mvua na sisi tuyatibu ili baadae tuyaelekeze katika bonde hili yaingie chini, yaani kama benki ya maji kwa ajili ya matumizi ya baadae na hii inakuwa tahadhari ili chanzo hichi kiwe na maji ya kutosha,” alisema Ngonyani.

Aliongeza kuwa Bonde la Wami/Ruvu ina jukumu kubwa la kuhakikisha wanahifadhi chanzo cha Mzakwe ili kiweze kufikia uhitaji wa kutosheleza mahitaji ya wakazi wa Dodoma wakati Wizara ya Maji wakitafuta chanzo kingine cha maji.

Alisema changamoto kubwa katika uhifadhi wa chanzo hicho ni shughuli za kibinadamu kama ufugaji ambapo ulizalisha sumu ambayo inakwenda kwenye maji na hiyo ni hatari kwa watumiaji.

“Watu wajifunze tukiongelea Wami/Ruvu sio Dar es Salaam tu, tunasimamia vyanzo vya maji hadi Dodoma.. Sisi kama Wami/Ruvu tunahakikisha chanzo hichi kinalindwa na kutunzwa kwa ajili ya kutoa maji yenye ubora na salama kwa matumizi ya wakazi wa Dodoma,” alisema Ngonyani.

Habari Kubwa