Mshiriki wa mkutano wa SADC aipa kongole MOI

21Aug 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Mshiriki wa mkutano wa SADC aipa kongole MOI

MSHIRIKI wa Mkutano wa 39 wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutoka nchini Botswana, Musa Dube, ameishukuru na kuipongeza Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) kwa huduma bora baada ya kutibiwa ugonjwa uliokua unamsumbua.

Dube ametoa keki ya shukrani kwa MOI kama sehemu ya shukrani kwa sababu ya  kuridhishwa na huduma bora alizopata.

Alikabidhi keki hiyo leo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Respicious Boniface, Dude amesema keki hiyo ni kama sehemu ya kuonyesha shukrani yake kwa uongozi na madaktari bingwa wa taasisi hiyo.

Keki hiyo ilikua na maneno yanayosema, “Thank you MOI” (Asante MOI) pamoja na bendera ya Botswana.

 “Sidhani kama maneno yanaweza kutosheleza shukrani zangu, asanteni sana kwa huduma nzuri, kwa kweli nimepata huduma vizuri, asante kwa kila aliyeshiriki kunitibu kuanzia mapokezi, Dk. Shabani, Dk. Mgisha, Dk. Violeth, Elius, Patrick, Josephine na wengine wote, asanteni,” amesema Dude

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface, amemueleza Dube kwamba MOI imekua ikitoa huduma kwa wananchi wa baadhi ya nchi za SADC hivyo kumuomba akawe balozi wa taasisi hiyo nchini Botswana.

“Tunakushukuru kwa kuamua kurudi kutushukuru kwa kukuhudumia, tunaimani kubwa kwamba wapo wengine watakuja kutibiwa Tanzania kwa sababu watasikia ulipata huduma bora hapa, wafikishie salamu waambie tuko tayari kuwahudumia pia” amesema Dk. Boniface 

Amesema MOI ilishiriki katika maonyesho ya wiki ya viwanda pamoja na mkutano wa 39 wa nchi za SADC ambao washiriki kutoka nchi mbalimbali walishangazwa na huduma bora zinazotolewa na MOI kwa gharama nafuu ambazo hazipo kwenye nchi zao.

Habari Kubwa