Msichana anayesumbuliwa ugonjwa wa ajabu asimulia

19Apr 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Msichana anayesumbuliwa ugonjwa wa ajabu asimulia

MKAZI wa Kitongoji cha Inung’una mkoani Singida, Mariam Rajab (25), mwenye kidonda mgongoni ambaye alionekana mtandaoni akiomba msaada wa matibabu na kupokelewa hospitali ya Muhimbili, amesimulia mateso makali aliyoyapata kwa miaka mitano.

Daktari Bingwa na Mkuu wa Idara ya Upasuaji katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Ibrahim Mkoma (kulia), akimfariji mkazi wa Singida Mariam Rajab Juma (25), aliyelazwa katika jengo la Kibasila Wadi namba 15, hospitalini hapo, jijini Dar es Salaam jana, akifanyiwa uchunguzi wa kidonda sugu kilichopo mgongoni kwake katika bega la kulia. Kushoto ni Ofisa Muuguzi wa Wadi hiyo, Yusta Nchemwa. PICHA: JOHN BADI

 

 

 

 

 

 Mariam ambaye alipokelewa usiku wa kuamkia jana Hospitali ya Muhimbili na sasa amelazwa wodi namba 15 jengo la Kibasila, amesimulia alivyoteseka na kidonda hicho ambacho chanzo chake ni moto.

Msichana huyo alisimulia kuwa miaka mitano iliyopita baada ya kuungua na moto eneo hilo la mgongo, alitibiwa hospitali ya Mkoa wa Singida hadi kilipoonekana kimepona.

Alisema baada ya kupona kovu la moto eneo hilo la mgongo lilitokea jipu ambalo baadaye lilipasuka.

“Lilipopasuka nikawa nakwenda hospitalini kusafishwa, lakini kadri siku zilivyoendelea kidonda kiliongezeka na gharama za kusafishwa kila siku ilikuwa ni Sh. 5,000, kama nilivyoeleza familia yetu ni maskini hivyo haikuweza kuzimudu,” alisema.

Mariam alisema aliendelea na huduma ya kusafishwa kila siku hospitali na kuanzia Agosti mwaka jana ilibidi awe anapewa huduma hiyo nyumbani na ndugu zake kutokana na hali ya kimaisha waliyonayo.

“Kadri kilivyokuwa kinasafishwa nyumbani kidonda kikawa kinaendelea kukua na mwisho wa siku kikafikia ukubwa huu, wakati nasafishwa nyumbani kuna mtu alituambia kuwa naweza kutumia unga wa dawa ya Flagyl kwa kuipaka hapo, hivyo nikawa nafanya hivyo,” alisema.

Alisema licha ya kuweka unga wa dawa hiyo kwenye kidonda mara baada ya kusafishwa, lakini haikusaidia zaidi kiliendelea kuongezeka ukubwa.

Alisema kutokana na hali ya kimaisha ya nyumbani ilifikia hatua marafiki zake aliosoma nao, walimchangia kiasi kidogo ambacho kilimuwezesha kununua baadhi ya vitu vilivyokuwa vinahitajika kwa ajili ya kukiosha kidonda hicho.

“Matumizi ya unga wa dawa hii haikuwa ushauri wa daktari, kuna mtu alituambia kuwa tukifanya hivyo kidonda kitapona hivyo kila siku nilikuwa nafanya baada ya kuoshwa,” alisema na kuongeza:

“Rafiki yangu ambaye nimesoma naye elimu ya sekondari alikuja kunitembea nyumbani na alipoona hali ninayopitia huku familia ikiwa haina fedha za kunitibu, alinishauri nirekodi video fupi ili niombe msaada kwa wasamaria wema mitandaoni ambayo ndiyo iliyomuwezesha kumfikisha hospitali ya Muhimbili,” alisema.

Mariam aliishukuru Hospitali ya Muhimbili kwa msaada huo walioutoa kwake kwa kumsafirisha kutoka Singida hadi hospitalini hapo na kumtibia bure.

“Naishukuru sana Hospitali ya Muhimbili kwa msaada walioutoa kwangu Mungu awabariki sana, wananitibia bure, wananihudumia kila kitu hadi chakula,” alisema.

Daktari Bingwa Mkuu wa Idara ya Upasuaji Hospitali ya Muhimbili, Ibrahim Mkoma, alisema kwa kawaida kidonda chochote kinachotokea kwenye kovu siyo cha kuchukuliwa kwa wepesi bali mhusika apelekwe hospitali.

Pia alisema mtu huyo akifikishwa hospitalini, wataalamu wasiishie kukisafisha bali walichunguze kama ni cha kawaida au saratani.

“Mara nyingi vidonda vinapotokezea kwenye kovu ni saratani na mara nyingi huwa kinaanza kama kiuvimbe alafu baadaye huwa na tabia kinapasuka na unatumia dawa hazisaidii, kadri unavyokisafisha ukikifungua unakuta kimeongezeka. Hivyo hali hiyo ikizidi miezi mitatu ujue hicho siyo kidonda cha kawaida,” alisema.

Dk. Mkoma alisema wameshaanza hatua za awali za matibabu baada ya kuona kidonda hicho chenye umri wa miaka mitano.

“Kwa historia Mariam akiwa na umri wa miaka mitano aliungua moto na jeraha lilipona, ndipo miaka mitano iliyopita kikaanza tena. Kutokana na historia ya kidonda hiki mara nyingi kidonda kinapotokea kwenye jeraha sugu tunachukulia kwa tahadhari kwa sababu siyo vya kawaida, kinaweza kikawa cha kawaida ama saratani,” alisema.

Alisema utaalam na uzoefu unaonyesha kidonda hicho siyo cha kawaida hivyo wamechukua sampuli ambayo imepelekwa maabara ambayo itatoa majibu kama ni saratani au la.

Alisema mara nyingi aina hiyo ya vidonda huwa ni saratani ambayo hutokea kwenye makovu ya vidonda vilivyotokea muda mrefu uliopita.

Dada wa pili kuzaliwa wa Mariam, Tatu Rajab, aliishukuru serikali kwa kuamua kutoa matibabu ya bure kwa mdogo wake kwa sababu maisha ya nyumbani ni duni na uwezo wa kumtibia kwa hatua aliyofikia hawakuwa nayo.

Kuhusu historia ya ugonjwa wa mdogo wake alisema baada ya kushindwa gharama za hospitali, walikuwa wakitumia pamba na yuso kumsafishia na baadaye walikuwa wakimpaka unga wa dawa ya fragin ili kuua bakteria.

“Kidonda hiki kimeibuka kwa mara ya tatu, mwanzo aliungua moto akapona ila baada ya miaka mitano mbele likatokea jipu tukalitumbua likashindikana kupona na alipopelekwa hospitali alifanyiwa upasuaji akakatwa nyama za paja akawekewa kwenye kidonda akapona nakumbuka ilikuwa mwaka 2015,” alisema.

Alisema baada ya hapo ndipo mwezi Agosti mwaka jana kikaanza upya na kutokana na familia kukosa fedha za matibabu wakawa wanakisafisha nyumbani hadi kilipofikia hatua hiyo ya sasa.

Alisema matumizi ya unga wa dawa hiyo yalitolewa na daktari mmoja ambaye alishauri awe anapakwa hapo ili kuua bakteria.

“Tulikuwa tunasaga dawa hizo mbili au tatu ndipo tunampaka kwenye kidonda. Mariam kabla ya kuugua alipomaliza kidato cha nne, alikuwa akijihusisha na biashara ya uuzaji wa nguo na wakati akiendelea na kazi hiyo ndipo alipoungua moto,” alisema.

Alisema Mariam ni mtoto wa nne kati ya watoto watano ambapo wa kike wapo wawili na kwamba baba yao ni fundi ujenzi na mama yao hana shughuli anayoifanya.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma na Huduma kwa Wateja hospitalini hapo, Aminiel Aligaesha, alisema kuwa mwanzoni mwa wiki hii picha ya Mariam ilisambaa mtandaoni akiomba msaada wa kufikishwa hospitali ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu.

Alisema Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alipoiona akatoa maagizo kwa uongozi wa hospitali ya Muhimbili atafutwe ili apelekwe hapo kwa ajili ya matibabu.

 

Habari Kubwa