Msimamo wa Spika kuhusu wabunge 19

17May 2022
Romana Mallya
DODOMA
Nipashe
Msimamo wa Spika kuhusu wabunge 19

SPIKA wa Bunge, Tulia Ackson, amesema Bunge haliwezi kuingilia mchakato wa mahakama kuhusu hatima ya wabunge 19 wa Viti Maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mpaka uamuzi wa jambo hilo utolewe mahakamani.

SPIKA wa Bunge, Tulia Ackson.

Akizungumza jana bungeni jijini Dodoma, Spika aliwaeleza wabunge kuwa hayo ndiyo maelezo yake kuhusu jambo hilo linaloendelea ikiwa kutakuwa na maswali yoyote msemaji wa jambo hilo yeye.

SAKATA LENYEWE

Akizungumzia kuhusu suala hilo, Spika Ackson alisema kuwa usiku wa Mei 11, mwaka huu, kupitia mitandao ya kijamii walipata taarifa kuwa Baraza Kuu la CHADEMA limeazimia kukubaliana na uamuzi wa Kamati Kuu ya chama wa kuwafukuza wabunge 19 wa Viti Maalum.

Alisema Mei 12, mwaka huu saa 7:15 na dakika 38 mchana kwa njia ya barua pepe alipokea barua za wabunge hao 19 wakimfahamisha kuwa uamuzi uliofikiwa na Baraza Kuu CHADEMA la kuwavua uanachama kwa sababu ya vitendo vyao vya kuteuliwa na kukubali kuwa wabunge wa Bunge sio halali.

“Kuwa ni kinyume cha katiba na hayakuzingatia haki ya msingi ya kuwasikiliza ama kuruhusu kujitetea na kwa mantiki hiyo wabunge wao wamepinga uamuzi huo na mwenendo mzima wa uamuzi uliofanyika ndani ya chama katika Makahama Kuu ya Tanzania Dar es Salaam, kupitia shauri namba 16 la mwaka 2022 namba 16/2022 dhidi ya Baraza la Wadhamini wa CHADEMA, Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” alibainisha.

Spika Ackson alisema tarehe hiyo hiyo saa 9:30 alasiri, Ofisa wa CHADEMA aliyejitambulisha kwa jina moja la Meshack alifika ofisi ndogo ya Bunge, Dar es Salaam kwa ajili ya kupeleka barua kwa Spika.

“Alipofika alielezwa na walinzi wa Bunge kuwa asubiri wafanye mawasiliano na kama wanaruhusiwa kupokea barua hiyo kwa kuwa wakati wa Bunge na maofisa wote wa ofisi ya Dar es Salaam huwa wanakuwa Dodoma.

“Wakati walinzi wanafanya mawasiliano hayo, ofisa huyo wa CHADEMA aliondoka bila kukabidhi barua hiyo na hii ni baada ya kupata maelekezo ya viongozi wa CHADEMA kwa simu kuwa wahusika hawawezi kupokea barua hiyo aondoke na watafanya utaratibu mwingine wa kuituma Dodoma.”

Alisema ilipofika saa 9:15 na sekunde 24 mchana na saa 9:19 na sekunde 41 mchana kupitia barua pepe walipokea barua yenye kumbukumbu namba C/HQ/ADM/PARA/33/37 iliyotiwa saini na John Mnyika ambaye ni Katibu Mkuu wa CHADEMA.

Barua hiyo, alisema ilikuwa ikimjulisha kwamba katika kikao chake Mei 11, mwaka huu, Baraza Kuu la chama lilipokea na kujadili rufani za walioitwa waliokuwa wanachama 19 ambao walikata rufani dhidi ya uamuzi wa kamati kuu, Novemba 29, mwaka 2020.

“Na kwamba Baraza Kuu la chama hicho kwa mujibu wa ibara ya 7.7.12 (f) ya katiba ya chama hicho ya mwaka 2006 toleo la mwaka 2019, limeazimia kukubaliana na uamuzi wa Kamati Kuu ya CHADEMA wa Novemba 17, 2020.

“Hivyo waliokuwa wanachama wa CHADEMA wameendelea kukosa sifa za kudaiwa kuwa wabunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania hivyo ni matumaini ya chama hicho kwamba itaufanyia kazi uamuzi wa Baraza Kuu la CHADEMA kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi.”

 

Spika alisema Mei 13, mwaka huu 2:42 asubuhi barua hiyo hiyo ilipelekwa kwa mkono ofisini kwake Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Singo Kigaila.

Pia, tarehe hiyo hiyo Mei saa 6:53 mchana barua hiyo iliwasilishwa tena kwake kwa njia ya DHL.

MSIMAMO

“Kwa mujibu wa katiba yetu mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano Tanzania ni mahakama, hivyo katika nchi yenye kuongozwa na msingi ya sheria na kuheshimiana kati ya mhimili mmoja na mwingine, Bunge haliwezi kuingilia mchakato wa mahakama na badala yake inalazimika kusubiri hadi hapo mahakama itakapotoa uamuzi wake kuhusu jambo hilo.

Alisema wabunge hao 19 walimtaarifu mapema Mei 12, mwaka huu kabla hajapokea taarifa yoyote rasmi kutoka CHADEMA kwamba wamekwenda mahakamani kwa ajili ya kulinda haki zao binafsi kama wanachama halali wa chama hicho na wabunge pamoja na kulinda katiba ya nchi na sheria ya taifa ya uchaguzi sura namba 343 iliyowafanya wao kuwa wabunge.

Alisema lazima wafahamu maelezo hayo yanatolewa kwa mujibu wa katiba, sheria walizozitunga Bunge.

“Hivyo, kwa kuzingatia misingi ya Katiba niliyoieleza ninalazimika kutotangaza kwamba nafasi za viti maalum vya wabunge 19 CHADEMA zipo wazi hadi hapo mahakama itakapokamilisha kazi yake ya kutoa uamuzi.

“Waheshimiwa wabunge hayo ndiyo maelezo yangu kuhusu jambo hili linaloendelea ikiwa kutakuwa na maswali yoyote msemaji wa jambo hili kuhusu wabunge hawa ni Spika.”

Akitolea ufafanuzi kuhusiana na suala hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari, Spika Tulia alisema Mahakama ikiwa na uamuzi wa jambo Fulani, mtu hawezi kusema hajui kwa sababu kesi ikifunguliwa, ni wajibu wa mtu kutafuta taarifa na si Mahakama kumwandikia muhusika.

“Nilivyojulishwa na wabunge 19 kwamba wamefungua kesi nilijiridhisha kesi ni namba ngapi na imefunguliwa Mahakama gani, kwa hiyo si suala la Mahakama kuniandikia. Ni  kazi yangu kutafuta taarifa,” alisema.

Alisema suala la kuwapo au kutokuwapo bungeni ni la kikatiba na kisheria.

 “Kama nilivyosema nasubiri uamuzi wa kisheria ukitoka kwasababu unaposema kikatiba,kisheria na kitaratibu ni kwamba vipo vifungu vinazungumzia hilo. Mahakama ikisema wamepoteza sifa ya kuwa wanachama kwa sababu chama kimewafukuza, kazi yangu ni moja tu kusubiri kutangaza nafasi kuwa wazi,” alisema.

Habari Kubwa