"Msingi wa maendeleo ya nchi ni maendeleo kwa wanyonge"- Kikwete

30Mar 2019
Frank Monyo
Nipashe
"Msingi wa maendeleo ya nchi ni maendeleo kwa wanyonge"- Kikwete

“Mkakati wa kuhakikisha maendeleo yanawafikia watu wa hali ya chini ndiyo msingi utaowafanya wananchi waendelee kuipenda na kuichagua CCM”

Maneno hayo ameyasemwa leo Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete alipokuwa anaweka jiwe la Msingi la ujenzi wa Zahanati ya Kitongoji Cha Chahua.

Baaada ya kuweka jiwe la msingi , Mh. Kikwete ameeleza furaha yake juu ya mafanikio ambao Halmashauri yake imepata kwa upande wa Afya,Elimu,Maendeleo ya Jamii na kusisitiza kuwa hayo yote yanatokana na msimamo ambao Chama chama chake kinasimamia hasa inapofika katika utekelezaji wa Ilani yake ambayo inawalenga kuwapelekea mabadiliko ya kweli wananchi wa hali za chini.

Mh. kikwete hakusita kueleza jinsi Raisi Magufuli anavyoendelea kupambana kuwasaidia Watanzania hasa katika kuwapatia huduma bora hasa kwa Upande wa Afya.

"Katika Halmashauri ya Chalinze tumejenga zaidi ya Zahanati 86 katika vitongoji na Vijiji ,Vituo vya Afya zaidi ya 13 na Sasa tunakamilisha Hospitali ya Wilaya ambayo fedha Kiasi cha Shilingi Milioni 500 zinatarajiwa kuletwa kumalizia Ujenzi pamoja na kununua vifaa tiba.

Tunachopaswa wana Chalinze wenzangu ni kuendelea kuunga mkono juhudi hizo ambazo Raisi Magufuli anafanya akishirikiana nami Mbunge wenu,Diwani wetu na Mwenyekiti wetu wa Kitongoji." amesema Kikwete na kuongeza;

“Katika Kata yetu ya Bwilingu, mambo mengi ya kimaendeleo tunayatekeleza ikiwa ni pamoja na kumalizia ahadi za Mheshimiwa Rais alizozitoa kipindi cha kampeni. Katika Upande wa Elimu ,tunapambana kupunguza wingi wa wanafunzi pale Shule ya Sekondari ya Chalinze kwa kumalizia shule ya sekondari ya pera na mkakati mwengine wa kuanzisha ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Chahua sambamba na ujenzi wa Maabara ya Kisasa katika kituo cha Afya Chalinze ili kusaidia vipimo vya ziada vya Kiafya.”amesema

Akizungumza kabla ya Mbunge kuweka jiwe la Msingi Mwenyekiti wa Kitongoji Bwana Sadallah Maisha amemshukuru Mbunge kwa msaada anaowasaidia watu wa Chahua hasa katika maendeleo ya kijamii.

“ Mheshimiwa Mbunge tunakushukuru kwa Kutupatia Nondo 80 na fedha taslimu zaidi ya Shilingi Milioni 2 pamoja na Nguvu zetu Wananchi."

Mbunge wa Chalinze anaendelea na Ziara ya kuangalia Shughuli za Maendeleo na Utekelezaji wa Ilani katika Vijiji,Kata na Vitomgoji mbalimbali Vya Halmashauri hiyo.

Katika Hali nyengine Mvua kubwa iliyonyesha kuanzia Alhamisi imeharibu Miundo mbinu katika Mji wa Chalinze na pera na Vitongoji mbalimbali.

Habari Kubwa