Msomi aeleza siri ya kukwama mipango, miradi ya maendeleo

15Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Msomi aeleza siri ya kukwama mipango, miradi ya maendeleo

KUKWAMA kwa utekelezaji wa miradi, sera na mipango mbalimbali ya maendeleo nchini baina ya  serikali na sekta binafsi, kunatokana na ukosefu wa elimu angalau shahada ya kwanza, imeelezwa.

Hayo yalibainishwa jana na Naibu Makamu Mkuu  wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), anayeshughulikia Taaluma, Prof. Deus Ngaruko, wakati wa mkutano kati ya wanataaluma wa chuo hicho na Kamati ya Fedha na Mipango ya Halmashauri ya Mji wa  Geita uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Profesa Ngaruko alisema uwepo wa wasomi wengi angalau wa shahada ya kwanza, unaweza kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo kutokana na maarifa yanayoweza kutumika kuikomboa jamii katika fani mbalimbali.

“Ili nchi iwe ya uchumi wa kati inatakiwa watu wake wanaoanza darasa la kwanza wanapata shahada ya kwanza angalau kwa asilimia 25, “ alisema.

Alisema hata azma ya kufikia uchumi wa viwanda kama nchi itakwenda kwa kasi ya asilimia nne au tano ya wasomi wenye shahada ya kwanza, itakwama mbele ya safari kama Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alivyoanzisha Ujamaa na Kujitegemea kutokana na watelekezaji waliopokea kuwa na elimu ya cheti na diploma.

Katibu Tawala Msaidizi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Mwangakala Sania, alisema wasomi ni muhimu katika kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.

“Sisi Halmashauri ya Mji wa Geita tumeamua kushirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ili kupata mawazo, ushauri wa kitaalamu juu ya azma ya kutekeleza miradi yetu ya maendeleo,” alisema.

Aidha, alisema utekelezaji wa miradi mbalimbali katika ngazi yoyote ya serikali unaongozwa na kanuni, sheria, sera na taratibu za kiserikali, hivyo kuwataka wasomi na watawala wa mradi huo kuvuta subira kwa ajili ya hatua hizo kutekelezeka.

Mchumi wa kutoka Halmashuri ya Mji wa Geita, Emmanuel Magesa, alishauri kuwapo kwa upembuzi yakinifu wa awali ambao utasaidia kupunguza gharama na pia uwezeshaji kwa viongozi wanaohusika kufanya uamuzi katika kuamua miradi hiyo kwa niaba ya wananchi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na jopo la madiwani wanane na viongozi watatu  kutoka Halmashauri ya Mji wa Geita ikiwa ni mwendelezo wa mikutano kati ya mkoa wa Geita na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika makubaliano ya kutekeleza miradi mbalimbali ya kuuendeleza mkoa wa Geita.

Habari Kubwa