Mtaalamu afichua helmenti pikipiki zilivyo hatari corona

24Mar 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Mtaalamu afichua helmenti pikipiki zilivyo hatari corona

TAHADHARI imetolewa kwa watumiaji wa usafiri wa pikipiki, maarufu bodaboda, kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa corona kutokana na kofia ngumu (helment) kuwa na uwezekano wa kusambaza virusi hivyo.

Kutokana na hatari hiyo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imewataka watumiaji wa usafiri huo kutumia kofia laini (disposable) kabla ya kuvaa kofia ngumu ili kujikinga dhidi ya maambukizo ya virusi hivyo.

Rai hiyo ilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi, Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma wa wizara hiyo, Dk. Amalberga Kasangala, alipozungumza na Nipashe kuhusu usalama wa watumiaji wa vyombo hivyo na tahadhari za kuchukua.

Aliwataka madereva kutochangia kofia moja na abiria ili kujikinga na maambukizo ya virusi hivyo ambavyo mgonjwa wa kwanza nchini aligundulika Machi 17 mwaka huu na tayari kulikuwa na watu 12 waliobainika kuugua ugonjwa huo hadi juzi.

“Madereva wa pikipiki wanatakiwa kuepuka kuchangia kofia moja na abiria ili kuepuka kupata maambukizo na kueneza zaidi kwa abiria wao. Ni muhimu wakahakikisha wanazingatia maelekezo yanayotolewa na wizara ili kuepuka kupata maambukizo,” alisihi.

Alisema kofia laini zikitumika kwa safari moja, zinatakiwa kutupwa ili kuepuka kupata maambukizo, akisisitiza kuwa kofia hizo ni salama zaidi kwa watumiaji hao.

Kuhusu abiria kutanguliza kofia za kawaida, kanga au mitandio kabla ya kuvaa kofia ngumu, mtaalamu huyo alisema siyo salama kwa sababu kama kofia aliyovaa itakuwa na virusi, ni rahisi kubaki kwenye nguo na mtumiaji kupata maambukizo.

“Kutumia kanga au mtandio ni hatari kwa sababu nguo zinaweza kubaki na virusi na kuendelea kutembea, labda kama unaweza kufua wakati huo huo kwa maji safi na sabuni. Hivyo ndiyo maana tunasisitiza ni muhimu kutumia kofia laini ambazo ukishatumia unatupa,” alisema.

Dk. Kasangala alisema watumiaji wa vyombo hivyo pia wanapaswa kutumia viziba midomo (masks), kusafisha mikono kwa vitakasa mikono (hand sanitizers) na kupeana nafasi wakati wanavyopanda ili kuepuka maambukizo.

Alisema watumiaji wa vyombo vyote vya usafiri wa umma wapo katika hatari ya kupata virusi kama hawatachukua tahadhari zinazotolewa kila siku ili kuepuka maambukizo mapya.

Aliwataka madereva wa pikipiki na bajaji kunawa mikono mara kwa mara, pindi wanapofikisha abiria na kabla ya kuchukua abiria mwingine.

Alisema madereva wa vyombo hivyo wanapaswa kuwa mabalozi wazuri wa kutoa elimu kwa abiria wanaowabeba kwa kuhakikisha wanazingatia maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Afya.

Habari Kubwa