Mtaka azungumza na wafanyabiashara wakubwa Dodoma

20Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe Jumapili
Mtaka azungumza na wafanyabiashara wakubwa Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, amekutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wakubwa mkoani Dodoma kwa lengo la kupokea maoni yao kuhusu mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji katika Mkoa huo.

Kikao hicho kimechofanyika kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, na kimejumuisha wafanyabiashara wakubwa kutoka sekta mbalimbali, Wakuu wa Taasisi zinazotoa huduma na zinazosimamia masuala ya biashara na uwekezaji zikiwemo Idara ya Kazi, Wakala wa Vipimo, TANESCO, TARURA, DUWASA, TIC, TRA, TBS, OSHA, TMDA na Viongozi wa Halmashauri ya jiji la Dodoma.

“Tukitaka Jiji la Dodoma liwe shindani ndani na nje ya jumuiya ya Afrika Mashariki, liweze kushindana na majiji kama Nairobi, Kampala, Bujumbura, Kigali na Majiji mengine makubwa nje ya Afrika, lazima Sekta Binafsi ijipambanue na kustawisha shughuli zake, na katika kipindi cha uongozi wangu kama Mkuu wa Mkoa wa Dodoma nitahakikisha Serikali inailinda Sekta Binafsi” amesema RC Mtaka.

Aidha, Mtaka amewataka wadau wa sekta binafsi katika Mkoa wa Dodoma kujipanga vyema ili kuweza kufaidika na fursa za kuwekeza zinazotokana na serikali kuhamishia shughuli zake katika Mkoa huo kama makao makuu ya nchi hata wanapokuja wawekezaji wakubwa kutoka nje ya nchi, sekta binafsi waweze kuingia nao mashirikiano katika uwekezaji mbalimbali.

Habari Kubwa