Mtambo wa kisasa kumaliza tatizo la vitambulisho taifa

02Apr 2020
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Mtambo wa kisasa kumaliza tatizo la vitambulisho taifa

SERIKALI imesema imepatia ufumbuzi wa malalamiko ya wananchi juu ya kuchelewa kwa vitambulisho vya taifa kwa kununua mashine mpya za kisasa zenye uwezo wa kufyatua vitambulisho 9,000 kwa saa.

Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene (kulia), akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dk. Anold Kihaule, wakati wa mkutano na waandishi wa habari, jijini Dodoma jana. PICHA: WMNN

Wakati suala la vitambulisho likipatiwa ufumbuzi, serikali imesema inakusudia kufanya mabadiliko makubwa ndani ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kutokana na utendaji usioridhisha.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alisema jana kuwa hatua hiyo imetokana na kubaini kuwa uchakavu wa mashine ndicho chanzo cha ucheleweshaji wa utoaji vitambulisho hivyo kwa wananchi.

Akizungunza na waandishi wa habari jijini hapa, Simbachawene alisema mashine hizo zilizonunuliwa kwa Sh. bilioni 8.5 zitakuwa mwarobaini kwa tatizo hilo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wananchi kwa muda sasa.

Pamoja na changamoto hiyo, alisema mpaka sasa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), imeshatoa vitambulisho milioni sita na kutambua wananchi milioni 21. 8 kati ya watu 27. 7 waliotarajiwa kusajiliwa.

Alisema namba za kipekee za utambulisho ni milioni 17. 8 zilikiwa zimezalishwa na zinaweza kutumika katika utambuzi wa watu.
Kwa mujibu wa Waziri, mashine hizo mpya zitakamilika kufungwa mwezi huu na kuanza kufanya kazi na kwamba baada ya hapo hakutakuwa na tatizo la kucheleweshwa kwa vitambulisho vya taifa.

Alisema mitambo mipya kwa kushirikiana na ile ya zamani, anaamini itatoa vitambulisho vingi na kwamba wanatarajia kukamikisha utoaji wa zana hizo ndani ya miaka miwili.

"Safarii hii vitambulisho vitakuwa bora. Awali vilivyotolewa havikuwa na ubora kutokana na mashine kuwa chakavu, " alisema Simbachawene huku akibainisha kuwa mtambo wa awali ulikuwa ukizalisha vitambulisho 500 kwa siku lakini kwa sasa vitaboreshwa na kuzalishwa vingi kwa siku.

Simbachawene aliwaomba radhi wananchi kutokana na kupata shida katika kupata vitambulisho na kuahidi kuwa kuanzia sasa watavipata kwa haraka bila usumbufu.

Katika hatua nyingine, Waziri Simbachawene alisema kutokana na utendaji usioridhisha, serikali inatarajia kufanya mabadiliko ndani ya Nida ili kuboresha.

Alisema pia watakuwa makini katika ugawaji wa vitambulisho kwa wageni wakaazi na wakimbizi.

Habari Kubwa