Mtambo wa kuvunja mawe kwenye mfumo wa mkojo waanza kazi

20Mar 2020
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Mtambo wa kuvunja mawe kwenye mfumo wa mkojo waanza kazi
  • Ni katika Hospitali ya Benjamini Mkapa ni wa kwanza Tanzania

MTAMBO wa kuvunja mawe kwenye mfumo wa mkojo hususan kwenye figo(Extracoporeal Shock Wave Lithotipsy), ambao ni wa kwanza nchini, umeanza kutoa huduma katika Hospitali ya Benjamini Mkapa.

Uvunjaji huo unafanywa kwa kutumia mionzi badala ya upasuaji.

Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Dk.Alphonce Chandika, alisema mtambo huo upo tayari kuanza huduma hiyo na kwa nchi nzima upo kwenye hospitali hiyo pekee.

“Tunashukuru serikali kwa kuleta vifaa tiba vya kisasa na vya gharama kubwa kwa ajili ya wananchi wake, tumekuwa tukitoa huduma ya upasuaji mawe kwa upasuaji, lakini huu mtambo unatumia mionzi ambayo si mikali sana,”alisema.

Aliongeza “Mgonjwa anawekwa kwenye mashine na inaelekezwa kwenye jiwe yenyewe ndio inapasua kwa kutumia mionzi na vipande hivyo vinatoka kwa njia ya mkojo.”

Aliishukuru serikali kwa kufunga mtambo huo wenye gharama ya Sh.Bilioni 2.5 na kwamba wamebaini  

Kanda ya kati inaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wenye mawe kwenye mfumo wa mkojo.

“Kwa takwimu za hospitalini hapa kwa wagonjwa wa mfumo wa mkojo zinaonesha wagonjwa wanaoongoza ni tezi dume inashika namba moja na inayofuatia ni mawe kwenye kibofu cha mkojo,”alisema.

Alieleza kuwa Hospitali hiyo inahudumia wagonjwa wanne hadi watano kwa wiki wenye mawe na kwa mwaka wagonjwa zaidi ya 50 wanafanyiwa upasuaji wa kuondoa mawe.

“Uwepo wa mashine hii ambayo imenunuliwa na serikali kwa gharama ya Sh.Bilioni 2.5 itasaidia wananchi wa kanda ya kati na watanzania wenye shida ya mawe kwenye kibofu cha mkojo,mawe yanasababisha figo kutofanya kazi, na mashine imewekwa ili kuokoa figo zisiharibike,”alisema.

Hata hivyo, alisema kunahitajika kufanya utafiti zaidi kujua sababu za kanda hiyo kuongoza kwa kuwa na wagonjwa wenye mawe lakini baadhi ya wataalam wanasema inasababishwa na hali ya hewa ya ukanda huo na watu kutokupenda kunywa maji.

Naye, Daktari Bingwa wa mfumo wa mkojo, Dk.Okoa Sukunala, alisema nchi zingine kwa wagonjwa wenye tatizo hilo upasuaji unafanyika chini ya asilimia moja lakini wanatumia mashine ya aina hiyo kusaga mawe.

“Njia tuliyokuwa tunatumia ilikuwa inamlazimu mgonjwa kulazwa wiki nzima wodini,”alisema.

Aidha, alisema zipo sababu mbalimbali ikiwemo ya kimazingira hasa mazingira ya joto na jangwa, tabia za watu kutokunywa maji ya kutosha, kurithi ambayo yanasababisha mawe kutengenezeka kwenye mfumo huo.

“Sababu nyingine ni umri miaka 20-40 ndo umri wa kutengeneza maji na wanaume ndio wapo kwenye hatari zaidi kupata mawe kuliko wanawake,”alisema.

Habari Kubwa