Mtaturu ashauri kupunguza utitiri wa kodi kwenye utalii

06Jun 2021
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe Jumapili
Mtaturu ashauri kupunguza utitiri wa kodi kwenye utalii

Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameishauri Wizara ya Maliasili na Utalii kupunguza utitiri wa Kodi zilizopo ambazo zimekuwa kikwazo kwa waendesha watalii nchini.

Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu.

Aidha, ameishauri wizara kukaa nao pamoja ili kuzungumza na kuweza kujua changamoto walizonazo na mahitaji yaliyopo katika sekta ya utalii.

Akichangia mjadala wa  bajeti ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2021/2022, Juni 5 bungeni, Mtaturu amesema kuna kampuni binafsi zinazotembeza watalii wanafanya kazi nzuri kwa niaba ya serikali na wao ndio wanakutana na watalii moja kwa moja hivyo ni vyema wakapewa nafasi ya kusikilizwa ili kueleza changamoto na mahitaji ya watalii.

""Lazima tujue watalii wetu wanataka nini cha kuwavutia zaidi,tusiwe tunaweka vitu kwa utashi wetu hii itakuwa ni sawa sawa na muuza duka kuuza nguo ya style fulani anazozipenda yeye badala ya kutafuta nguo wanazozipenda wateja, niwaombe mkae na Tour Operators waweze kuwaambia taste ya watalii ikoje na wanataka nini,"

Akizungumzia kuhusu utitiri wa Kodi na tozo amesema,"Katika sekta hii kuna tozo 20 ambazo zimekuwa kikwazo,ni vizuri zikaangaliwa upya,tunajua Kodi inasaidia kuboresha maisha ya wananchi lakini ni vizuri walipe Kodi kwa furaha ili Kodi hiyo iwe endelevu."

Habari Kubwa