Mtia nia ya urais aahidi kuisuka upya TAKUKURU

11Jul 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Mtia nia ya urais aahidi kuisuka upya TAKUKURU

WAKILI wa Mahakama Kuu, Simba Richmomd Akaro, amechukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania urais wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akiahidi kusuka upya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) endapo atafanikiwa kukalia kiti hicho.

Wakili Simba alikabidhiwa fomu hiyo jana kwenye Ofisi za Makao Makuu ya CHADEMA jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho, Reginald Munisi.

Baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, Wakili Simba alitaja mambo atakayoyafanya endapo atapitishwa na CHADEMA kugombea nafasi hiyo na kushinda kuwa ni pamoja na kuboresha vyombo vinavyosimamia haki.

Alisema uboreshaji huo utaigusa moja kwa moja TAKUKURU ambayo kwa mtazamo wake anaona kwa sasa haiko huru katika kupambana na wala rushwa nchini.

Vilevile, Wakili Simba alisema akifanikiwa kupitishwa na CHADEMA kugombea urais wa Tanzania kisha kuchaguliwa na Watanzania kuwaongoza, atahakikisha maendeleo na demokrasia vinaenda pamoja.

"Tusiwe tunaongelea maendeleo bila demokrasia. Ukiwa na moja tu ni ulemavu, ni muhimu kwamba demokrasia na maendeleo viwe vinakwenda sambamba," alisema.

Aliishauri CHADEMA kutowapa nafasi ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kupitia chama hicho, wanasiasa walioshika nafasi za uongozi serikalini kwa muda mrefu, kwa maelezo kwamba wamechokwa na wananchi.

Wakili Simba anakuwa mtia nia wa sita ndani ya CHADEMA kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu tangu kuanza kwa mchakato huo Julai 4, ukitarajiwa kufungwa Julai 19 mwaka huu.

Waliochukua fomu awali ni Makamu Mwenyeketi wa chama hicho, Tundu Lissu, Dk. Mayrose Majinge, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu, Wakili Gaspar Mwalyela, aliyekuwa Meya wa wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwitta na Leonard Manyama, aliyechukua fomu juzi jioni.

Habari Kubwa