Mtifuano mpya wa CCM, Ukawa

08Jan 2017
Richard Makore
Nipashe Jumapili
Mtifuano mpya wa CCM, Ukawa

WAKATI zikiwa zimebaki siku 14 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani wa kata 20 nchini, kumeibuka dalili za kuibuka kwa mtifuano mpya baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mahasimu wao wakuu, muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Hali hiyo imebainika kutokana na mikakati ya kusaka ushindi iliyowekwa wazi na pande zote mbili, CCM ikisisitiza kuendeleza kampeni kali kuhakikisha kuwa inashinda katika maeneo yote yanayowaniwa huku Ukawa wakidai kushitukia njama zinazoweza kuwaponza baadhi ya wagombea wao na hivyo kutangaza njia za kukabiliana na hali hiyo. Vyama vinavyounda Ukawa ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.

Katika uchaguzi huo utakaofanyika Januari 22, CCM na vyama vinavyounda Ukawa wanatarajiwa kuchuana na vyama vingine kadhaa katika kuwania ubunge wa Jimbo la Dimani visiwani Zanzibar na pia udiwani katika kata 20.

Akizungumza na Nipashe jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, alisema wamejianda kwa kampeni kabambe kuhakikisha kuwa wanafanya vizuri.

Polepole alisema ili kutimiza malengo yao, watawatumia viongozi wao wa kitaifa kunadi sera zao kwenye maeneo yote.
Katibu huyo hakutaja majina ya viongozi watakaohusika katika kampeni hizo, ingawa aliongeza kuwa kuanzia kesho, watatoa ratiba kamili itakayoonyesha kila kiongozi amepangiwa eneo gani la kushambulia.

Alisema CCM imejipanga vyema kimkakati kuhakikisha wanashinda katika kata zote 20 za Tanzania Bara na pia kutetea nafasi ya ubunge wa Jimbo la Dimani, Zanzibar iliyokuwa ikiongozwa na marehemu Hafidh Ali Tahir aliyefariki Novemba, mwaka jana. Tayari Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alishaanza kazi baada ya kuzindua kampeni za chama hicho kwenye Jimbo la Dimani, juzi.

Hata hivyo, wakati Polepole akieleza hayo, Ukawa wameeleza kile wanachodai kuwa ni kushitukia uwezekano wa kuwapo kwa hujuma kwa kurubuniwa wagombea wao katika baadhi ya maeneo ili wajitoe na hivyo, wamejipanga kukabiliana na hilo kwa kusimamisha wagombea zaidi ya mmoja kutoka kambi yao kwenye baadhi ya maeneo.

Naibu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Mbarala Maharagande, alisema Ukawa wamekubaliana kuwa kila chama kisimamishe mgombea ili kukwepa uwezekano wa kuwapo kwa hujuma ili mwishowe kuwapa nafasi mahasimu wao kupita kirahisi.

Maharagande aliongeza kuwa katika utekelezaji wa mpango huo, wameamua kuwa kila mgombea atakuwa tayari kuendelea kuwawakilisha pindi ikitokea jambo hilo likafanikishwa na mahasimu wao. Maharagande hakuwataja moja kwa moja mahasimu wanaowahofia kuwa wanaweza kuwahujumu, ingawa inafahamika wazi kuwa wanaochuana nao zaidi ni CCM.

Hata hivyo, Maharagande hakufafanua pia sababu za wao kuwa na hofu hiyo ya kuwapo kwa mchezo mchafu, jambo linaloashiria uwezekano wa kuwapo kwa mtifuano mpya baina ya pande hizo ikiwa ni takribani mwaka mmoja sasa tangu kuchuana kwao vikali katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015.

MAALIM SEIF, LOWASSA KUTIKISA LEO
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye ndiye aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa, anatarajiwa kuungana na aliyekuwa mgombea urais wa kambi hiyo visiwani Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad kuzindua kampeni za kumnadi mgombea wao wa ubunge katika Jimbo la Dimani, Abdulrazak Khatib Ramadhan wa CUF. Lowassa na Maalim Seif watazindua kampeni hizo kwenye viwanja vya Skuli ya Fuoni.

Akizungumzia kampeni hizo, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF (Zanzibar), Salum Bimani, alisema Ukawa wameendelea kuonyesha mshikamano mkubwa katika kipindi hiki ili kuhakikisha kuwa wanapata ushindi.

Alisema licha ya kuwapo maneno ya hapa na pale yenye nia ya kuwavuruga, wameendeleza umoja na ndiyo maana wamejitosa katika uchaguzi huo kwa nia ya kulitwaa Jimbo la Dimani.

Aidha, kuhusiana na kampeni za maeneo yote kwa ujumla, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumain Makene, aliliambia Nipashe kuwa watashambulia katika maeneo yote, wakiwa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Lowassa.

Aliwataja viongozi wengine watakaohusika katika kampeni hizo kuwa ni wajumbe wa kamati kuu ya Chadema wakiwamo Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Prof. Mwesiga Baregu na Tundu Lissu. Watakuwamo pia viongozi wengine kadhaa wa kitaifa, kanda, jimbo, kata na hadi kwenye matawi.

Alisema kampeni hizi zitakuwa za aina yake kwa kuwa viongozi wote wataacha ofisi zao na kuvamia kata zinazofanya uchaguzi ili kuhakikisha wanawanadi wagombea wao. Tayari Sumaye alishaanza kampeni mkoani Pwani, jana.

Makene alisema Chadema watatumia fursa ya kufanyika kwa kampeni hizo kutoa ujumbe mzito kwa wananchi, hasa baada ya kutopata nafasi hiyo kwa muda mrefu tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu uliopita.

RATIBA UCHAGUZI
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza ratiba ya uchaguzi mdogo katika kujaza nafasi kupitia Vyama vya Siasa na Wananchi wote katika nafasi za ubunge na udiwani kwa mujibu wa vifungu vya 37 (1) (b) na 46 (2) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343; na Vifungu vya 13 (3) na 48 (2) vya Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292. Kampeni za uchaguzi huo zinatarajia kuhitimishwa Januari 21 mwaka huu na uchaguzi utafanyika Jumapili ya Januari 22, mwaka.

Habari Kubwa