Mto Msimbazi kujengwa kwa bil. 200/-

15May 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mto Msimbazi kujengwa kwa bil. 200/-

CHANGAMOTO ya mafuriko katika bonde la Mto Msimbazi, inatarajiwa kufika kikomo baada ya serikali kuahidi kuanza kufanya upembuzi yakinifu mwezi ujao kwa kuanza ujenzi.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akiwa katika ziara ya kukagua athari za mafuriko katika eneo la msimbazi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, wakati alipofanya ziara ya kukagua athari za mvua katika eneo la Jangwani, alisema tayari Sh. bilioni 200 zimeshatolewa kama mkopo na Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya kazi hiyo.

Alisema maeneo yote ya bonde hilo yataboreshwa kwa kujengwa majengo ya miundombinu ya kisasa ili kuondokana na changamoto ya mafuriko yanayoleta athari kwa wananchi na wakazi wa maeneo hayo.

“Kuanzia mwezi ujao tutaanza kufanya upembuzi yakinifu kwaajili ya ujenzi wa bonde la mto Msimbazi wenye urefu wa kilometa 19 na tayari fedha zipo kwa ajili ya kazi hiyo,” alisema Makonda.

Alisema pia serikali imeanza kufanya ukarabati wa miundombinu iliyoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha ikiwamo madaraja, barabara, mito na mifereji.

Aidha, Makonda aliwapa pole wananchi waliokumbwa na athari za mafuriko wakiwamo ambao mali zao zimeharibiwa na wengine kulazimika kuyahama makazi yao.

Makonda pia aliwataka wananchi wanaoishi maeneo hatarishi kuhama huku akiwataka wakazi wa jiji hilo kufanya usafi katika mazingira yao ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.

Kwa upande wa wananchi wanaoishi Jangwani, walilieleza Nipashe kuwa, serikali imekuwa ikitoa ahadi hewa ya kuboresha bonde hilo.

Mmoja wa wananchi hao, Jumanne Mrisho alisema, hawapo tayari kuhama kwa sababu serikali imekuwa ikiwafukuza na kuwabomolea nyumba zao bila kufanya muendelezo wowote katika eneo hilo.

“Sisi tumekaa Jangwani kwa muda mrefu, lakini hakuna siku ambayo serikali imeliendeleza eneo hili. Kama wameahidi watajenga waje ila hatutaondoka mpaka tuwaone wakifanya kazi,” alisema Mrisho.

Mwaka jana Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, alikaririwa na vyombo vya habari akisema ndoto yake ni kuona eneo la Mto Msimbazi linaboreshwa na kuwekwa vivutio mbalimbali, maeneo ya kupumzika, maduka na hoteli kupitia fedha zitakazotolewa na Benki ya Dunia.

Agosti mwaka jana, Mhandisi Mshauri Mussa Nati, aliwasilisha andiko la utekelezaji wa mradi uboreshaji wa bonde hilo katika mkutano wa udhibiti wa maafa hatarishi uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema utafiti uliofanyika unaonyesha kuwa baadhi ya makazi ya watu yataondolewa ili kupisha ujenzi wa mradi huo ambao utawezesha maji kwenda katika mkondo wake hadi baharini.

Nati alisema mradi huo ulianza kwa kutambua eneo lenye tatizo, namna ya kupunguza kwa kuishirikisha jamii na wataalamu, kufundisha jamii na kuandaa wataalamu wa baadaye pamoja na mitaala kwa ajili ya kutumika kwenye vyuo mbalimbali nchini.

Mwaka 2015, Baraza la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (Nemc), liliendesha bomoabomoa kwa wakazi wa eneo la Bonde la Msimbazi, Kinondoni, ikiwa ni pamoja na maeneo mengine ya usawa wa mto Msimbazi na nyumba zaidi ya 150 zilibomolewa.