Mtoto adai alimwona baba wa kambo akimuua mamaye

04Jul 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Mtoto adai alimwona baba wa kambo akimuua mamaye

MTOTO Hassan Hussein (10) amedai mahakamani katika kesi ya mauaji ya mama yake mzazi, Bahati Hussein, kwamba alimwona baba yake wa kambo, Godfrey Nkwambi, akimnyonga mama yake na kumwamuru asipige kelele.

Mtuhumiwa Godfrey Nkwambi, anayekabiliwa na kesi ya mauaji ya mkewe, akiwa chini ya ulinzi wa askari Magerezakatika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana, baada kumaliza kusikiliza ushahidi wake.PICHA: HELLEN MWANGO

Ushahidi huo aliutoa jana mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Pamela Mazengo, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, iliyopewa mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Hassan ambaye alilala chumbani kwa mama yake (wakati huo akiwa na miaka mitano), alidai kuwa siku ya tukio alimwona baba yake wa kambo ni mshtakiwa katika kesi hiyo, alitoa madai hayo wakati akitoa ushahidi dhidi ya mauaji hayo.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Erick Shija, shahidi huyo alidai siku ya tukio akiwa amelala  chumbani kwa mama yake chini kwenye godoro pamoja na mdogo wake aliyemtaja kwa jina la Ibrahim, kwa kawaida  mama yake na baba yake wa kambo walikuwa wakilala kitandani.

Siku ya tukio, alidai kuwa usiku alishtuka na alimuona mshtakiwa (baba wa kambo) akimnyonga mama yake  na alimwambia asipige kelele na mama yake alikuwa akitikisa miguu huku akitoa sauti kwa mbali.

"Nililala lakini niliposhtuka nilimwona mshtakiwa  akifanya hivi halafu hivi (alionyesha mahakama mikono ya mshtakiwa  ilivyokuwa imeshika kichwa na kidevu na kukizungusha). Mama alikuwa akipiga miguu kitandani na kutoa kelele kwa mbali, God aliniambia  nisipige kelele, mimi nikanyamaza, nikamwona akitoka nje sikujua kilichoendelea kwani niliendelea kulala hadi asubuhi," alidai Hussein.

Alidai kuwa asubuhi  alimwacha mama yake akiwa bado amelala, yeye akatoka nje kupiga mswaki  na baadaye alikwenda kucheza.

"Siku hiyo sikumwona  Godfey na sikujua alikokwenda lakini  baadaye nilisikia watu wakilia nyumbani kwetu, ndugu zangu wakaniambia mama yetu mzazi amefariki (dunia)," alidai shahidi huyo na kusababisha ndugu wa marehemu waliofika mahakamani  kusikiliza kesi hiyo kuanza kutoa machozi.

Shahidi mwingine ni mtoto wa marehemu, Khadija Abibu (15), aliieleza mahakama kuwa mama yake alifariki dunia Juni 21, 2014 na kwamba Juni 20 alipotoka kucheza alikuta baba yake (mshtakiwa), mama yake na watu wengine wakiwa wamekaa katika mkeka nyumbani kwao Ulongoni.

Alidai kuwa dada yake anayeitwa Hadija Shabani, alimwambia kuwa kulikuwa na ugomvi kati ya baba na mama yake ambao ulisuluhishwa na kwisha na baadaye alimshuhudia mshtakiwa akimpa fedha mama yake akanunue mboga kwa ajili ya chakula cha usiku.

Alidai kuwa majira ya saa 5:00 usiku, alikwenda kuwalaza wadogo zake, Hassan na Rahim, chumbani kwa mama yao na kisha akaenda kulala chumbani kwake  pamoja na mtoto wa mama yake mdogo.

"Usiku nilishtuka nikasikia mama na Godfrey wanagombana. Mtoto wa mama mdogo alikuwa anaogopa, nikamwambia yataisha sisi tulale, tukabaki macho kitandani. Mtoto  wa mama mdogo akabanwa na haja ndogo, hivyo tukatoka nje kujisaidia," alidai Khadija.

Alidai kuwa walipotoka nje walimwona Godfrey akiwa amekaa katika kochi sebuleni akiwa amevaa kipensi, shati begani huku akitokwa na jasho na kuwahoji wanakokwenda.

"Sisi tulimjibu tunaenda kujisaidia, akasema haya. Tuliporudi tukasikia Godfrey akifungua mlango wa sebuleni na kutoka nje, sisi tulijificha nyuma ya mlango wa sebuleni, tulimsikia Godfrey akimgongea mpangaji wa chumba cha nje na kumuuliza kama alisikia kelele, yule mpangaji akamwambia hakusikia kelele," alidai shahidi.

Shahidi huyo alidai, baadaye walienda kulala, asubuhi aliamshwa na mama mwenye nyumba ambaye alimtaka achukuwe beseni la vyombo apeleke chumbani kwa mama yake.

Huku akitokwa na machozi, shahidi huyo alidai  aligonga mlango lakini mama yake hakuitikia na alipoingia ndani alimkuta mama yake amelala akiwa amefunikwa shuka jeupe na kanga kichwani, alimtikisa hakuamka na kutoka nje huku akipiga kelele.

"Nilikuta mama kalala, niliendelea kumwamsha bila mafanikio, nikamfunua alikuwa hajavaa nguo, nikamshika kifua kuona kama roho yake inadunda, ilikuwa haidundi, nikatoka nje nikipiga kelele. Mama  mwenye nyumba aliniuliza nikamwambia mama yangu hahemi amefunikwa nguo, majirani walikuja na kumwangalia, wakasema atakuwa amezimia, wakamvalisha nguo na kumpeleka hospitalini," alidai.

Khadija alidai kuwa watu waliorudi kutoka hospitalini walimwambia kuwa mama yao amekufa na alinyongwa. Alidai kuwa mama yake alinyongwa na Godfrey kwa sababu alishawahi kumtamkia kuwa atamuua yeye na familia yake kwa kuwa hataki kuiona.

"Mama pia alishawahi kunambia kwamba, 'mwanangu nikifa Godfrey ndiye kaniua," alidai.

Naye shahidi Khadija Shabani, ambaye alikuwa akimwita marehemu shangazi, aliieleza mahakama kwamba wawili hao walikuwa na ugomvi na kwamba Godfrey alikuwa akimtuhumu Bahati kuwa na uhusiano wa kimapenzi na jirani yao.

Habari Kubwa