Mtoto alivyouawa kikatili, mtuhumiwa mmoja ashikiliwa

26Jul 2021
Said Hamdani
Lindi
Nipashe
Mtoto alivyouawa kikatili, mtuhumiwa mmoja ashikiliwa

MTOTO Mwilu Ahamadi (6) mkazi wa Kijiji cha Nampungu, Kata ya Mingumbi, Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, amekutwa amekufa baada ya kutoweka nyumbani kwao wiki moja iliyopita, huku baadhi ya viungo vya mwili wake vikiwa vimeondolewa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, ACP Mtatiro Kitinkwi, amethibitisha kutoa kwa tukio hilo na kueleza kuwa wanamshikilia mtu mmoja kutokana na kifo cha mtoto huyo.

Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, waliojitambulisha kwa majina ya Hemedi Ismail, Mohamed Juma na Elena Emmanuel, wameeleza kwamba mtoto huyo alitoweka nyumbani tangu Julai 15, mwaka huu.

Walisema siku hiyo mtoto huyo akiwa anacheza na wenzake, aliondoka nyumbani kwao na hakuweza kurejea tena.

Walisema kwamba kitendo cha kutorejea nyumbani kwa mtoto huyo, wananchi walianza kumtafuta maeneo mbalimbali bila mafanikio.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nampungu, Kassimu Macho, alithibitisha kupotea kwa mtoto huyo na kueleza kuwa alipatikana Julai 21, mwaka huu, akiwa amefariki huku baadhi ya viungo vyake vikiwa vimeondolewa.

Alitaja viungo vilivyoondolewa ni pamoja na sikio la kulia na mguu wa kulia ambavyo vimekatwa.

Macho alisema mwili wa mtoto huyo ulionekana baada ya baba mdogo wa mtoto huyo, Hemedi Chauleni, kupandisha mashetani na kumtaka mdogo wake aliyetajwa kwa jina la Seifu waende moja ya njia zilizopo katika kijiji hicho na kufanikiwa kuukuta mwili wake ukionekana umenyongwa shingo.

‘‘Baada ya kumtafuta kwa siku zote tano bila mafanikio, baba mdogo wa yule kijana, ghafla akapandisha mashetani na kumtaka Issa ampeleke upande huu,” alisema Macho.

Alisema Hemedi Chauleni, ndiye aliyesaidia upatikanaji wa mwili wa mtoto huyo baada ya kupandisha mashetani, hata hivyo Jeshi la Polisi linamshikilia kwa mahojiano zaidi.