Mtoto atuhumiwa kumuua mama kwa kumkaba shingo

04Jun 2020
Restuta Damian
Bukoba
Nipashe
Mtoto atuhumiwa kumuua mama kwa kumkaba shingo

JUSTINE Joseph, mkazi wa Kijiji cha Omungando, wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera, anatuhumiwa kumuua mama yake mzazi, Theopista Joseph (72), kwa kumshambulia kwa kipigo na kumkaba shingo hadi kufa.

Kamanda wa Polisi mkoani hapo, Revocatus Malimi, picha mtandao

Kamanda wa Polisi mkoani hapo, Revocatus Malimi, amethibitisha tukio hilo la mauaji kuwa, Mei 5, mwaka huu saa tatu usiku, mtuhumiwa alimvamia mama yake akiwa njiani kurudi nyumbani na kuanza kumgombeza kwa kutomhudumia mgonjwa nyumbani.

Malimi alisema polisi ilifanya uchunguzi wa awali baada ya mtuhumiwa kukimbia kusikojulikana na kubaini kuwa baba wa familia hiyo, ambaye ni baba mzazi wa mtuhumiwa aliugua kwa kipindi kirefu ugonjwa wa kiharusi.

Alisema, mkewe (marehemu) anadaiwa kutomuuguza vizuri mume wake, badala yake alimuacha ndani na kwenda kunywa pombe vilabuni licha ya kushauriwa na mtuhumiwa asiende kunywa.

"Marehemu alishauriwa na mtuhumiwa ambaye ni mwanawe kwamba asiende kunywa pombe jambo lililokuwa likimpa hasira, kwa sababu ya kutokaa nyumbani kumpatia huduma baba yake," alisema Malimi.

Katika tukio lingine Kamanda Malimi alisema Juni mosi, majira ya saa tatu usiku kijijini Igabilo, wilayani Muleba, yalitokea mauaji ya Happiness Ibrahim (33), yaliyosababishwa na kipigo cha mume wake, Hamis Luge (36).

Alisema chanzo cha mauaji hayo ni kutoelewana na mume wake aliyemtaka kuacha kunywa pombe na kurudi nyumbani ili yeye aende kuvua samaki mwaloni.

"Kwa uchunguzi wa awali mtuhumiwa aliacha amemzuia mke wake asiendelee kunywa pombe, lakini mke alikaidi na kuendelea kunywa hadi mume wake aliporudi saa 2:00 usiku na kumkuta bado yuko kilabuni," alisema Malimi.

Alisema mtuhumiwa alimfuata mkewe kilabuni na kumtaka waondoke kurudi nyumbani, lakini mke aligoma.

Kamanda aliendelea kueleza kuwa mtuhumiwa alimchukua kwa nguvu mkewe badi nyumbani na kuanza kumpiga hadi kumsababishia kifo baada ya kuzidiwa na kipigo ambacho kilisababisha majeraha kichwani.

Habari Kubwa