Mtoto auawa kikatili mwili wakutwa hauna viungo

12Oct 2018
Happy Severine
BUSEGA
Nipashe
Mtoto auawa kikatili mwili wakutwa hauna viungo

MWANAFUNZI wa darasa la kwanza wa Shule ya Msingi Mwabasabi iliyoko kijiji cha Lamadi, wilayani Busega mkoani Simiyu, Susana Shija (9), amekutwa amekufa na mwili wake kutupwa kwenye pagala.

Mwili wa mtoto huyo ambao ulikutwa ukiwa hauna baadhi ya viungo, uligundulika juzi saa nne asubuhi.

Baadhi ya viungo ambavyo havikukutwa ni pamoja na mikono na miguu yote na kunyolewa nywele zake zote kichwani.

Mama mzazi wa marehemu, Dina Halili, alisema mtoto wake alitoweka nyumbani katika mazingira ya kutatanisha wiki mbili zilizopita na walitoa taarifa kituo cha polisi Lamadi.

Alisema baada ya mtoto huyo kupotea walimtafuta kwa kushirikiana na polisi, lakini hawakumpata hadi jana alipopewa taarifa kuwa mwili wa mtoto wake umekutwa kwenye nyumba hiyo.

"Nilipofika eneo la tukio nilibaini kuwa ni mtoto wangu, inaonekana aliteswa sana na kuondolewa viungo hivyo na kutupwa hiyo sehemu muda mrefu, maana mwili wake ulikuwa tayari umeanza kuharibika," alisema Halili.

Baadhi ya mashuhuda walisema walikuta mwili wa mtoto huyo ukiwa katika hali mbaya kutokana na kukaa muda mrefu katika eneo hilo.

Mmoja wa mashuhuda, Mussa Mathias, alisema walikuta mwili wa mwanafunzi huyo ukiwa umetelekezwa kwenye moja ya chumba cha jengo hilo ambalo ni pagala.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Maua Ntengwasabuni, alisema taarifa walizopata kutoka kwa wazazi wa marehemu ni kwamba enzi za uhai wake mtoto huyo alikuwa akitoroka nyumbani mara kwa mara.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Duesdedit Nsemeki, alisema mwili wa mwanafunzi huyo uligunduliwa na mmiliki wa nyumba hiyo.

"Tunajiuliza maswali mengi hapa kwanini wazazi hawakutoa taarifa polisi baada ya mtoto wao kupotea na alipotea zaidi ya siku 10, tuko katika uchunguzi wa jambo hilo, lakini tayari mwili wa marehemu umezikwa," alisema Kamanda Nsimeki.

Alisema polisi wanafanya uchuguzi wa tukio hilo linalohusishwa na imani za kishirikina kutokana na marehemu kutokukutwa na baadhi ya viungo vyake.

Habari Kubwa