Mtoto Mkulima atuma salamu

09Mar 2018
Paul Mabeja
Nipashe
Mtoto Mkulima atuma salamu

WAZIRI Mkuu mstaafu katika serikali ya awamu ya nne, Mizengo Pinda maarufu Mtoto wa Mkulima, ametaka viongozi katika ngazi mbalimbali kuwa waadilifu badala kuwa wabinafsi, waeneza chuki na wala rushwa.

WAZIRI Mkuu mstaafu katika serikali ya awamu ya nne, Mizengo Pinda.

Mtoto wa Mkulima alitoa rai hiyo jana alipokuwa akifunga kongamano la kidini la kuliombea taifa na viongozi mbalimbali ndani ya serikali.

Alisema kuwa ili pawe na taifa lenye viongozi wazuri wasihojihusisha na vitendo vya rushwa na hatimaye utawala bora, ni lazima kupata viongozi ambao ni wacha Mungu na wenye hofu.

Pinda alisema viongozi ndani ya serikali, vyama vya siasa na taasisi mbalimbali ni lazima wafanye kazi zao kwa hofu ya Mungu kutoka moyoni na siyo maigizo.

"Viongozi kama watafanya kazi zao kwa uadilifu ni wazi kuwa kila mwananchi ataweza kujivunia na kujiongezea kipato kutokana na rasilimali zinazotokana na vyanzo mbalimbali ambavyo Mungu ameviweka katika nchi yetu," alisema Pinda.

Aidha, Pinda ambaye alikuwa Waziri Mkuu kati ya Februari 9, 2008-Novemba 20, 2015 alisema kuna haja ya kuanzishwa kwa vikundi vya maombi kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu.

Maombi hayo yalikuwa pia na lengo la kuweka njia bora ambayo watoto watakuwa waaminifu katika utendaji wao wa kazi, kwa misingi ya kujitenga na ufisadi, rushwa pamoja na ubadhirifu wa mali za umma.