Mtoto wa betri arejea shuleni

21Sep 2016
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Mtoto wa betri arejea shuleni

HAPPINESS John (5), aliyefanyiwa upasuaji Julai 15, mwaka huu na kuwekewa betri ndani ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ameripoti shuleni Hill Creast English Medium mjini Arusha kuendelea na masomo yake ya awali.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, mama wa mtoto huyo, Elitruda Malley, alisema mwanaye aliripoti jana shuleni na anaendelea vizuri kiafya.

"Ni jambo la kumshukuru Mungu, mwanangu anaendelea vizuri tangu tutoke Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu, amerejea shuleni kuendelea na masomo yake ya awali baada ya kukatiza wakati akiumwa," alisema Malley.

Mtoto huyo alilazimika kukatiza masomo yake ya awali baada ya kuwa akipoteza fahamu mara kwa mara anaposhtuka, kucheza sana na wenzake na kuishiwa nguvu pamoja na kutokula chakula vizuri.

Happiness amewekewa betri katika moyo baada ya kufanyiwa upasuaji unaojulikana kitaalamu kama ‘Pacemaker Insertation' ili kusaidia mapigo ya moyo wake kuwa katika hali ya kawaida.

Alifanyiwa upasuaji huo ili kuongeza kasi ya mapigo ya moyo wake yaliyokuwa 20-60 kwa dakika mpaka kati ya 60-80 kwa dakika inavyopaswa kuwa katika mfumo wa damu wa binadamu.

MASHARTI MAGUMU
Baada ya upasuaji huo, atahitajika kuishi kwa masharti ambayo ni pamoja na kutocheza michezo ya hatari na watoto wenziwe, kutochezea sumaku na kutoishi jirani na maeneo yenye minara ya simu, masharti ambayo mama yake anatakiwa kuyasimamia.

Mtoto huyo pia hatakiwi kufanyiwa ukaguzi kwa vifaa vyenye mionzi, ikiwamo kwenye viwanja vya ndege. Amekabidhiwa kadi ya muda inayomruhusu kutokaguliwa.

MRI HAIFAI PIA

Daktari Bingwa wa Masuala ya Mionzi, Musa Ndukeki, akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, alisema wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa aina hiyo, hawaruhusiwi kuchunguzwa kwa kutumia kipimo cha mashine ya Magnetic Resonance Imaging (MRI) kwa kuwa inahatarisha usalama wao.

Alisema MRI inatumia sumaku na si mionzi, hivyo kifaa chochote kilicho na chuma ambacho amekivaa mgonjwa nje au ndani ya mwili, hakiruhusiwi anapofanyiwa vipimo kwa kutumia mashine hiyo.

"Mgonjwa aliye na chuma mwilini, aliyewekewa betri katika moyo, aliyevaa hereni, saa, cheni, haruhusiwi kuingia navyo katika mashine hii. MRI ikikutana na chuma itakachofanya ni kukivuta kwa nguvu, hata kama ni saa, itavuka mkononi," alisema Dk. Ndukeki.

Alisema iwapo mgonjwa aliyewekewa betri au chuma katika sehemu ya mwili wake, hasa waliopata ajali, hutumia matibabu mbadala iwapo kuna ulazima wa kuwafanyia uchunguzi zaidi katika miili yao.

Baada ya kuruhusiwa JKCI, Elitruda alikabidhiwa CD ambayo ina maelezo muhimu kuhusu matibabu pamoja na hatua za kuchukua iwapo Happiness atapata dharura yoyote kabla ya kurejea tena JKCI Oktoba, mwaka huu.

"Mama yake tumemkabidhi CD yenye maelekezo, atakaporejea baada ya miezi mitatu tangu aruhusiwe, Happiness atahitajika kutumia kadi maalum ya kimataifa ambayo inatambulika, ili asipitishwe katika maeneo ya ukaguzi yanayotumia mionzi kama viwanja vya ndege," alifafanua Mohamed Maulid, Msemaji wa JKCI.

Alisema kwa sasa Happiness hahitaji matibabu ya aina yoyote kutokana na betri aliyokuwa nayo kuhitaji zaidi uangalizi.

Habari Kubwa