Mtoto wa marehemu Shekh Yahaya atoa utabiri wake wa mwaka 2017

09Jan 2017
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
Mtoto wa marehemu Shekh Yahaya atoa utabiri wake wa mwaka 2017

MTOTO wa Marehemu Sheikh Yahya Hussein, Maalim Hassan Yahya Hussen ametabiri mwaka 2017 kuwa ni mwaka ambao viongozi wa kisiasa na dini watakumbwa na kashfa ya ngono na fumanizi itakayo kusababisha fedhea na anguko katika tasnia zao.

Maalim Hassan Yahya Hussen.

Aidha amewatoa wasiwasi waandishi wa habari ambao walitabiriwa kifo ifikapo Machi mwaka huu na Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) Ubungo Jijini Dar es Salaam, Anthony Lusekelo kwa sababu waliandika habari zake baada ya kukamatwa na Polisi, kuwa hawatakufa kwani yeye hayupo karibu na Mungu kama walivyo Askofu Kadinal Pengo na Mchungaji Malasusa.

Maalim Hassan, alitoa utabiri huo jana jijini Dar es Salaam, na kudai kuwa mwaka 2017 utakuwa ni mwaka kwa viongozi wa dini kutoa mataamshi ya kutatanisha ambayo yanaweza kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani na utulivu.

Alisema kuwa mwaka 2017 unaotawaliwa na nyota ya Simba unahashiria vifo vya viongozi wa kubwa na maarufu wa kisiasa na kidini nchini kufa ghafla, vifo hivyo vitatokana na msongo wa moyo na mawazo au shinikizo la damu.

Alisema pia mwaka 2017 utakuwa ni mwaka wa viongozi wa dini, kisiasa, taasisi za kiserikali, binafsi na za umma kujiuzulu nyadhifa zao kutoka na kashfa za kiuongozi.

“Pamoja na jitihada za Rais John Magufuli kudhibiti mianya ya rushwa inaonekana kuwa katika mwaka huu kasi ya ufisadi na rushwa itakayofanywa na viongozi wa kisiasa na maafisa tawala na wakurugenzi itaongezeka zaidi,”alisema Hassan

Vile vile Maalim Hassan, alisema kuwa mwaka huu viongozi wa kubwa wa vyama vya upinzani duniani ikiwamo Tanzania watarejea kwenye vyama walivyovihama.

Na kuongeza kuwa mwaka 2017 ni mwaka ambao itashuhudiwa muanguko wa vyama tawala katika nchi mbalimbali duniani na kwamba viongozi wa nchi kadhaa duniani kutoa matamshi ya ajabu yatakayowashangaza wananchi wa nchi zao.

“Pia mwaka 2017 kutakuwa na ajali nyingi ambazo zinawahusu wanasiasa watawala na viongozi wa dini, sambamba na kifo cha chama kimoja maarufu cha siasa hapa nchi,”alisema Hassan

Aliongeza kuwa katika mwaka huu pia kutatokea vifo vya gafla vya kawaida kwa wasanii maarufu duniani na Tanzania ikiwamo, ambavyo vitatokana na fumanizi kuuliwa au kuuwana wenyewe.

Pia mwaka 2017 kutakuwapo na ajali nyingi kuwakuta wanasiasa, watawala na viongozi wa dini, sambamba na kuzama kwa meli kwenye moja ya bahari kuu duniani na Denge moja ya taifa kubwa kuanguka na hivyo kusabisha vifo vya watu kadhaa.

Alisema kuwa mwaka 2017 utashuhudiwa na mioto mingi na mikubwa hapa nchini na duniani ambayo itasababisha madhara makubwa, pia kutokea kwa mafuriko yatakayoleta vifo na madhara mengine makubwa.

“Vifo na maafa haya niliyoyatabiri yanaweza yasitokee iwapo watu wataacha rabsha na uharaka wa kufanya mamabo kama nyota ya mwaka 2017 inavyosema watu waache chuki binafsi, choyo, kuchongeana na ngono isiyokubalika kisheria,”alisema Hassan

Alisema kuwa pamoja na baadhi ya viongozi wa siasa kudai kuwa nchi imeingia katika wimbi la njaa, amedai kuwa mwaka 2017 utakuwa ni wa neema kwa watakaojikita katika masuala ya kilimo na hakutakuwa na njaa kwani kutakuwa na chakula cha kutosha.

Alifafanua kuwa mwaka 2017 umeanza siku ya jumapili.Kwa mujibu wa utabiri siku ya jumapili inashabihishwa na sayari ya jua ambapo ina nyota ya Simba ambayo asili yake ni Moto, pia huonesha kuwa ni Ufalme, utawala na uongozi wa kisiasa na kidini.

Alisema pia mwaka unaoanza jumapili mara nyingi huwa ni mwkaa wa kijicho, watu hasa wanasiasa, viongozi wa dini na familia kuoneana husuda na watu wa kada hiyo hujikuta wakikumbwa na vifo vya kawaida au vya kuuawa au kuuana.

“Haya yote ninayotabiri yanatokana na umbile la mwaka 2017, ukiondoa namba 20 inabadi 17 ambapo kitaaluma namba 1 inaashiria nyota ya Punda (Aries) inayotawaliwa na sayari ya Mars ambayo asili yake ni moto na inahusika na Mashaka, vita, hiyana,nishati, maudhi, hujuma, mikosi, kuvunja vitu, migogoro bughudha na watu kufanya au kufanyiwa mambo mabaya,”alisema.

Aliendelea kusema kuwa namba 7 ni nyota ya mizani, na sayari yake ni (Venus) ambayo asili yake ni hewa na inahashiria muafaka, urafiki, uzuri wa moyo, mapenzi, ndoa na masikilizano, mapatano, tabia nzuri mambo ya muziki na wasanii starehe, michezo mahakimu, mawakili wanasheria na wanawake.

Alisemna kuwa ukijumlisha namba (1) na (7) utapata namba (8) ambayo asili yake ni sayari ya Mars ambayo inatawala nyota ya N’ge ambayo asili yake ni maji.

Aidha alisema kuwa watu wanatakiwa kumtegemea Mungu zaidi katika mambo yao yote katika mwaka 2017 kama anavyofanya Rais Magufuli kumweka mbele Mungu katika mambo yake yote kwa maana hiyo yeye atasalimika na uhasama huo.

Habari Kubwa