Mtoto wa miaka 5 akutwa malipo ya korosho

16May 2019
Na Mwandishi Wetu
 MTWARA
Nipashe
Mtoto wa miaka 5 akutwa malipo ya korosho

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Mtwara, imewafikisha mahakamani watuhumiwa wawili akiwamo mfanyakazi wa benki ya NMB Wilaya ya Nanyumbu kwa kuingiza jina la mtoto mwenye umri wa miaka mitano katika malipo ya korosho.

Watuhumiwa hao wanashtakiwa kwa makosa ya kugushi na utakatishaji wa fedha.

Wanadaiwa kwa udanganyifu huo kujipatia Sh. milioni tano kinyume na sheria za nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mtwara, Stephen Mafipa, alisema watuhumiwa hao ni Juma Mbevu, ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama cha Ushirika cha Napacho Amcos na Agustino Nziku, ambaye ni mfanyakazi wa benki ya NMB, Wilaya ya Nanyumbu, ambao ilidaiwa kuwa walishirikiana kufanya kosa hilo.

Alisema watuhumiwa kwa pamoja wanashtakiwa kwa makosa ya kula njama, kutenda makosa na kutumia nyaraka zenye maelezo ya uongo kumdanganya mwajiri kinyume na vifungu namba 32 na 22 vya Sheria ya Kuzuia na kupambana na rushwa.

Alisema jina la mtoto wa mtuhumiwa Augustino Nziku, ambaye ni mfanyakazi wa benki ya NMB, Wilaya ya Nanyumbu liliingiziwa kwenye orodha ya malipo huku wakijua mtoto huyo hastahili kuuza korosho hivyo kumwezesha mtuhumiwa kujipatia kiasi cha Sh. milioni tano ambazo hakustahili.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi imefunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, eneo ambalo watuhumiwa walitenda kosa hilo.

Alisema kesi zingine za udanganyifu katika malipo ya korosho bado zinaendelea kuchunguzwa na zikikamilika wahusika watafikishwa katika vyombo vya sheria.

Habari Kubwa