Mtuhumiwa akiri mahakamani kufanya biashara ya binadamu

08Mar 2019
Stephen Chidiye
Tunduru
Nipashe
Mtuhumiwa akiri mahakamani kufanya biashara ya binadamu

MKAZI wa Wilaya ya Tunduru, Fatuma Alli (35), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Wilaya, kujibu tuhuma za kujihusisha na biashara ya kuuza binadamu.

Akimsomea shtaka hilo, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Bosco Kilumbe, alidai kuwa mtuhumiwa huyo alifanya kosa hilo kati ya Februari 28 na Machi Mosi, mwaka huu.

Alidai kuwa katika tukio hilo, mtuhumiwa huyo alinaswa akiwa anawatorosha wanafunzi akiwamo wa kidato cha kwanza wa Shule ya Nandembo mwenye umri wa miaka 14 (jina linahifadhiwa).

Kwa mujibu wa mwendasha mashtaka, wasichana wengine ambao walikuwa wanatoroshwa na mtuhumiwa huyo ni mwenye umri wa miaka 15, wa kidato cha kwanza na wa kidato cha pili mwenye umri wa miaka 16 (wote majina yao yanahifadhiwa).

Kilumbe aliendelea kufafanua kuwa kwa kufanya hivyo mtuhumiwa huyo alifanya kosa kinyume na kifungu cha sheria namba 4 (1) pamoja na kifungu namba 5 cha Sheria ya Kuzuia Biashara ya Binadamu namba 6 ya mwaka 2008.

Mtuhumiwa alikiri kufanya kosa hilo na kujitetea kuwa alifanya hivyo akiwa anatekeleza maelekezo aliyopewa na mume wake aliyemtaja kuwa ni Hamisi Kanju, ambaye alidai kuwa alimwagiza ampelekee wasichana watakao msaidia kufanya biashara ya kuuza mgahawa.

Kutokana na mtuhumiwa huyo kukiri mashtaka yake, Hakimu Janneth Kaluyenda, aliamuru kesi hiyo ianze kusikilizwa Machi 21, mwaka huu, kwa kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa Jamhuri.

Mtuhumiwa yuko rumande kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo yalimtaka kuwa na wadhamini wawili na kati yao akiwamo mtumishi wa serikali na mkazi wa Tunduru.

Habari Kubwa