Mtuhumiwa ujambazi auawa kwa panga

06Mar 2017
Elisante John
SINGIDA
Nipashe
Mtuhumiwa ujambazi auawa kwa panga

MTU anayesadikiwa kuwa jambazi aliyekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40, ameuawa baada ya kuzidiwa nguvu wakati akiwa kwenye jaribio la wizi ndani ya nyumba ya mkazi wa Kijiji cha Tupendane Wilaya ya Ikungi mkoani humu.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani humu, Isaya Mbughi, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 1:30 usiku baada ya mtuhumiwa huyo kuingia ndani ya nyumba ya Juma Rashid, mkazi wa Kijiji Tupendane, katika Wilaya ya Ikungi mkoani humu.

Kamanda Mbughi alisema mtuhumiwa huyo akiwa na wenzake, walifanikiwa kuvunja mlango wa nyumba ya Rashid.
Alisema mtuhumiwa huyo aliingia ndani ya nyumba hiyo akiwa na panga.

Hata hivyo, Kamanda Mbughi alisema mtuhumiwa huyo alizidiwa nguvu na wanaume wawili aliowakuta ndani ya nyumba hiyo ambapo alikatwa panga shingoni na kufariki dunia kutokana na kuvuja damu nyingi.

Alisema watu wawili akiwamo mmliki wa nyumba hiyo, Juma Rashid na Ibrahim Hassan, wametiwa mbaroni na wanaendelea kuhojiwa na polisi.

Kamanda Mbughi alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha kifo hicho baada ya mtuhumiwa huyo akiwa na wenzake kuvamia nyumba hiyo kwa lengo la kujipatia mali isivyo halali.

Alitoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kwenda katika Hospitali ya Puma iliyopo Ikungi ambako mwili wa mtuhumiwa huyo umehifadhiwa kwa ajili ya kuutambua.

Habari Kubwa